AZAM FC 3-1 JKT Tanzania

AZAM FC 3-1 JKT: TUMEFUNGA MWAKA KIBABE

Azam FC imeufunga mwala 2024 kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya timu ngumu ya JKT Tanzania. Ikiwa nyumbani, Azam Complex, Azam FC ilijikuta ikitanguliwa kwa bao la mapema la dakika ya 13 kwa mkwaju wa adhabu ndogo wa Said Khamis Ndemla.

Lakini mnamo dakika ya 36, Pascal Msindo, akaisawazishia Azam FC akitumia vizuri pasi ya bahati mbaya kutoka kwa Gibril Sillah kufuatia mlinda mlango wa JKT Tanzania Yakoub Suleiman Ali, ‘kuosha’ vibaya na mpira kuangukia kwa Sillah.

Hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili, Azam FC ilicharuka ikitafuta ushindi na mnamo dakika ya 63 Idd Seleman ‘Nado’ akafunga bao la pili akitumia vizuri pasi murua ya Feisal Salum ‘Feitoto’. Lusajo Mwaikenda alipiga pasi ndefu kwenda kwa Gibril Sillah, lakini raia huyo wa Gambia akagundua kuwa ameotea hivyo akauacha mpira uende zake.

Ndipo Feisal Salum alipoutokea kwa kasi ya ajabu na kumzidi mbio na maarifa mlinzi mmoja wa JKT Tanzania na kupiga majaro ya ‘cut back’ yaliyomkuta Nado aliyeukwamisha mpira wavuni kwa shuti kali la chini chini akiwa juu ya kidoti cha kupigia penati cha JKT Tanzania.

Maelewano ya Idd Nado na Feitoto yaliendelea kuwaelemea na kuwavuruga kabisa JKT Tanzania na kujikuta wakiruhusu bao la tatu mnano dakika ya 72. Feitoto alipiga kona ya ‘cut back’ kama yale majaro ya bao la pili, na Idd Nado akiwa nje kidogo ya 18 akapiga shuti la chini chini lililomshinda kipa wa JKT Tanzania, Yakoub Suleiman Ali.

Hadi dakika 90 zinakamilika, Azam FC ilikuwa mbele kda mabat 3-1.

Baada ya mchezo huu ligi itasimama hadi mwezi wa tatu, kupisha Mapinduzi Cup na baadaye kambi ya timu ya taifa kujiandaa na CHAN na kissa CHAN yenyewe itakayofanyika Februari katika nchi za Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda.

Results

Club1st Half2nd HalfGoalsOutcome
AZAM FC123Win
JKT Tanzania101Loss