Katika kuendelea kujiweka sawa kabla ya kurejea kwa ligi kuu, Azam FC itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar dimbani Azam Complex, Januari 31, 2025, saa moja kamili usiku.
Akiongea na tovuti hii, meneja wa Azam FC Rashid Said Mgunya, amesema mchezo huo ambao ni wa mwisho kabla ya kuwavaa KMC katika muendelezo wa ligi kuu ya NBC, utamsaidia mwalimu kujua maendeleo ya kiufundi ya wachezaji wake hadi sasa.
“Kocha wetu Rashid Taoussi, anataka kuwapima wachezaji wake kuona wameelewa kiasi gani maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa mazoezini tangu kusimama kwa ligi. Tumeshacheza mechi tatu na zote zilimsaidia kubaini kitu na sasa anataka kujiridhisha kama wachezaji wamshika mafunzo sawasawa”, alisema Rashid.
Huu utakuwa mchezo wa nne wa kirafiki kwa Azam FC tangu irudi mazoezini baada ya kutoka kwa taarifa ya kurejea mapema kwa ligi kuu, tofauti na ratiba ya awali kwamba ligi ingerejea Machi.
Ilicheza na Mtibwa Sugar, Januari 19, huko Manungu Turiani Morogoro na kupoteza 1-0. Ikashinda 3-2 didi ya JKT Tanzania pale Meja Isamuhyo Januari 25 na kushinda 3-2 aisha ikamalizia na Uhamiaji ya Zanzibar, Januari 28 pale Azam Complex na kushinda 6-0.
Mchezo ujao wa ligi kuu kwa Azam FC utakuwa dhidi ya KMC, Februari 6, 2025 dimbani Azam Complex.