Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya vijana chini ya miaka 17, Azam FC, wameendeleza ubabe wao kwa ushindi wa nne mfululizo msimu huu baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 4-1 kwenye viwanja vya kituo cha maendeleo ya ufundi cha TFF Kigamboni jijini Dar Es Salaam.
Azam FC iliuanza mchezo huo kwa kasi ikitafuta mabao ya mapema ambapo dakika ya pili tu ya Mohamed Shillah aliachia shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Ruvu Shooting na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 16 ya mchezo kiungo Abdallah Salum aliumia na kutoka, na nafasi yake kuchukuliwa na Azam Mkasa. Japo mabadiliko hayo hayakuwa ya kiufundi lakini yaliongeza nguvu kwenye safu ya kiungo na dakika ya 21, Mohamed Shillah akaifungia Azam FC bao la kwanza akipokea pasi ya Adinan Rashid.
Dakika tano baadaye, yaani dakika ya 21 ya mchezo, Mohamed Shillah akafunga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Ikram Aman. Hili likawa bao la tatu kwa Shillah, ambaye ni nahodha wa timu hiyo.
Dakika ya 37 Mohamed Shillah akageuka kuwa mpishio wa mabao pale alipotoa mujarabu kwa Adinan Rashid aliyefunga bao la tatu. Bao hilo likadumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili hakikuanza vizuri kwa Azam FC kwani Ruvu Shooting walikuja juu kutafuta mabao ya kusawazisha. Walipeleka mashambulizi kadhaa langoni kwa Azam FC lakini safu ya ulinzi ikiongozwa na Pius Severin na Rajab Said ilisimama imara kuhakikisha kipa Abdulrahman Vuai hapati rabsha rabsha zozote.
Baada ya kuona ni vigumu kuipenya ngome, Ruvu Shooting wakageukiwa mbinu ya kupiga mashuti ya ambapo ambapo dakika ya 60 Abubakar Juma aliifungia timu yake bao la shuti la mbali lililomzidi kipa wa Azam FC aliyekiuwa amesogea mbele kidogo.
Bao hilo ni kama likawaamsha Azam FC na kuuchukua mchezo na kupeleka mashambulizi langoni mwa Ruvu Shooting na dakika ya 75 Migel Joel Mlokozi akaifungia Azam FC bao la nne akiunganisha mpira uliokuwa ukirudi baada ya kuokolewa shuti la awali.
Hadi mwisho wa mchezo, Azam FC 4-1 Ruvu Shooting.
Hadi sasa Azam FC ina alama 12 baada ya mechi nne, ikifunga mabao 13 na kuruhusu bao moja.
Kocha wa timu hiyo, Mohamed Juma Badru akiuzungumzia mchezo anasema vijana wake walicheza kwa kiwango alichotarajia lakini amesikitishwa na bao waliloruhusu. Hilo ni bao la kwanza kwao kufungwa kwenye mashindano ya msimu huu.
Naye mfungaji wa mabao mawili, Mohamed Shillah, ambaye ni nahodha, amesema ushindi huu ni mzuri kwao katika kuhakikisha wanaifikia au kuipita rekodi ya wenzao waliyoiweka msimu uliopita.
Shillah ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha msimu uliopita kilichobeba ubingwa kwa kushinda michezo 11 na kutoa sare mchezo mmoja tu, anasema anaiona timu ya msimu huu ikiimarika kidogo kidogo na inaelekea kuwa kama ile ya msimu uliopita.
Kikosi
Abdulrahman Vuai, Abdallah Salum, Ismail Ally, Pius Severin, Rajab Said, Migel Joel, Adinan Rashid, Ikram Aman, Issa Abdallah, Mohamed Shillah, Peter Zogora
Akiba
Hassan Juma, Albogast Charles, Ismail Issa, Gideon Paul, Azam Mkasa, Rashid Abdallah, Aman Fonest, Ally Nawanda, Mwinshehe Ally