Lusajo Mwaikenda na Prince Dube ndiyo wachezaji waliotufungia mabao yetu muhimu kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Simba SC dimbani Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mabao hayo yakatuvusha hadi fainali ya mashindano hayo na kutufanya tufikie hatua hiyo kwa mara ya tatu katika historia ya miaka 8 ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Kupitia makala hii, tunakuletea makala maalumu kuhusu mashujaa wetu waliotufungia mabao siku ile.

LUSAJO MWAIKENDA

Jina lake kamili ni Lusajo Elikaga Mwaikenda. Alizaliwa Oktoba 27, 2000 mjini Dar Es Salaam ambako anaishi hadi sasa. Ni zao la akademi yetu aliyojiunga nayo mwaka 2018 akiingia moja kwa moja timu ya chini ya miaka 20 na majukumu yake ya kwanza yalikuwa Kombe la Uhai, mashindano yaliyofanyika Dodoma, kwenye viwanja vya chuo kikuu cha UDOM.

Azam FC ilitolewa kwenye nusu fainali na Stand United na pia kuikosa nafasi ya tatu kwa mikwaju ya penati mbele ya Simba. Baada ya mashindano kijana akarudi Chamazi na kuendelea kujinoa chini ya Meja Mingange, aliyekuwa kocha wa timu za vijana wakati huo.

Msimu wa 2019/20 akapandishwa timu ya wakubwa na baadaye kutolewa kwa mkopo kwenda KMC. Akadumu huko kwa misimu miwili na akarudi nyumbani msimu wa 2021/22.

Nyakati zote hizo alikuwa akicheza kama mlinzi wa kati, na hata mwanzo wa msimu wa 2021/22 alianza kama mlinzi wa kati akitengeneza pacha yake na Daniel Amoah.

Lakini baadaye kocha George Lwandamina akambadilisha nafasi na kuanza kumtumia kama mlinzi wa kulia, akianza kwenye mechi dhidi ya Pyramids ya Misri, kwenye kombe la Shirikisho la Afrika.

Katika mechi zote mbili, ya Chamazi iliyomalizika kwa sare ya 0-0 na ya Cairo iliyomalizika kwa Azam FC kupoteza 1-0, Lusajo alionesha uwezo mkubwa akimdhibiti nyota Ramadhan Sobhi ambaye alinunuliwa na Pyramids kutoka ligi kuu ya England.

Kuanzia hapo akapitishwa rasmi kuwa beki wa pembeni hadi sasa anavyoipeleka Azam FC kwenye fainali.

PRINCE DUBE

Nchini Zimbabwe alipewa jina la Mgadafe lakini Tanzania akabatizwa majina mengi sana. Kwanza lilikuwa Mwanamfalme, ikiwa ni tafsiri ya moja kwa moja ya jina lake la Prince. Lakini baadaye akaitwa ‘Muuaji Anayetabasamu’ au Smiling Assasin, kutokana na madhara anayowapatia makipa wa timu pinzani huku uso wake muda wote ukipambwa na tabasamu la upole.

Alizaliwa Februari 17, 1997 mjini Bulawayo nchini Zimbabwe na kuanzia soka lake kwenye akademi ya klabu ya Highlanders ya huko. Msimu wa 2016/17 alipandishwa timu ya wakubwa na kufanya vizuri kiasi cha kuivutia klabu ya Super Sport United ya Afrika Kusini kumsaini msimu wa 2017/18.

Hata hivyo mambo hayakumuendea vizuri na lilipofika dirisha dogo msimu huo huo akatolewa kwa mkopo kwenda Black Leopards ya huko huko Afrika Kusini. Mkopo wake ulipoisha mwishoni mwa msimu, akaamua kurudi nyumbani Zimbabwe kwenye klabu yake ya utotoni, Highlanders.

Akajipanga upya na kurudisha makali yake na Disemba 2019 akaivutia klabu ya Shaanxi Chang’an Athletic iliyokuwa ikishiriki League One, sawa na kwanza, ikamualika kwa majaribio. Akaenda kufanya na akafanikiwa, akarudi nyumbani kusubiri taratibu zingine zifuate.

Lakini bahati mbaya ndipo ukazuka ugonjwa wa UVIKO 19 na China ikafunga mipaka yake, ndipo dili likafa. Hadi hapo, Ligi ya Zimbabwe ilikuwa imemalizika na wanasubiri msimu mpya uanze, mwezi Machi kama ilivyokuwa kawaida yao.

Mlipuko wa UVIKO 19 ukasababisha msimu mpya wa soka nchini Zimbabwe, 2020, usianze na ikambidi akae nyumbani kwa miezi sita bila kucheza. Akiendelea kuwa nyumbani ndipo Azam FC ikatokea na kumnasa, Agosti 2020.

Dube aliuanza msimu kwa kuweka alama yake inayomfanya aendelee kuheshimika hadi sasa ambapo yeye ni mmoja wa wachezaji maarufu nchini na vipenzi vya mashabiki wa timu zote.

Hao ndiyo wauaji wa Nangwanda.

Tukutane Mkwakwani.