Kutokana na sababu za kiusalama, ziara ya Azam FC nchini Kenya kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia FC, imefutwa. Kwa mujibu wa barua kutoka Gor Mahia iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Raymond Oruo, kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin MohmedAmin, maarufu kama Popat, ziara hiyo imefutwa hadi taarifa nyingine itakapotolewa.

Wikendi iliyopita, Azam FC ilipokea mwaliko kutoka Gor Mahia kwenda Nairobi, Kenya, kwa ajili ya mechi moja ya kirafiki ambayo ilipangwa kufanyika Machi 26 kwenye uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Azam FC ipo katika maandalizi kabambe kwa ajili ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Mtibwa Sugar. Kuelekea mechi hiyo, benchi la ufundi lilihitaji mechi mbili za kirafiki ili kupima utayari wa wachezaji kwa ajili ya mechi hizo kutokana na mazoezi ambayo wamekuwa wakiyafanya. Zaid ya Gor Mahia, mechi nyingine ni dhidi ya JKU a,mbayo ilipangwa kufanyika Machi 22 dimbani Azam Complex. Mechi hiyo itakuwepo kama ilivyopangwa.