Machi 26 mwaka huu Azam FC itakuwa mgeni wa Gor Mahia FC kwenye mchezo wa kirafiki wa kiufundi ndani ya dimba la Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya. Azam FC inatarajiwa kuondoka jijini Dar Es Salaam Jumatano ya Machi 24 kwa basi, ikipitia Arusha.

Mechi hii inafuatia mwaliko kutoka Gor Mahia, timu ambayo imeshakutana na Azam FC mara mbili huko nyuma. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye fainali ya Kombe la Kagame mwaka 2015 jijini Dar Es Salaam, ambapo Azam FC ilishinda 2-0.

Mabao mawili ya nahodha John Bocco na winga kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche, yalitosha kuipatia Azam FC ubingwa wao wa kwanza wa Afrika Mashariki. Alianza Bocco dakika ya 16 pale alipomalizia kazi mujarabu ya Kipre Tchetche. Kipindi cha pili, dakika ya 20 au dakika ya 65 ya mchezo, Kipre akafunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo wa umbali wa yadi 25 na kuihakikisha Azam FC ushindi huo.

Mara ya pili ikwa mwaka 2018 kwenye nusu fainali ya mashindano hayo hayo ya Kagame, jijini Dar Es Saalam na Azam FC kushinda tena 2-0 kwa mabao ya dakika za ziada kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90 za kawaida.

Ditram nchimbi alifunga bao dakika 93 kwa shuti la chini chini akiuwahi mpira uliokuwa ukizagaa zagaa ndani ya eneo la hatari la Gor Mahia baada ya shuti la Joseph Kimwaga kuwababatiza walinzi wa timu hiyo. Dakika saba baadaye, Bruce Kangwa alifunga bao la juhudi binafsi akikokota mpira kuanzia mita chache kutoka katikati ya uwanja hadi kwenda kufunga.

Pia hii itakuwa mara ya pili kwa Azam FC kufanya ziara ya kifundi nchini Kenya. Mara ya kwanza ilikuwa Januari 2013 ambapo ilikaa Kenya kwa wiki moja na kucheza michezo mitatu ya kirafiki kwenye uwanja wa Nyayo.

Mwaka 2013 Azam FC ilifanya ziara ya wiki moja nchini Kenya na kucheza mechi tatu za kirafiki. Mechi ya kwanza ilikuwa ya kipigo cha 2-1 kutoka AFC Leopards katika siku ambayo Azam FC ilipata penati tatu lakini mbili zilikoswa, na kufungwa moja. Mabao ya Leorpads yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa na lile la Azam FC lilifungwa na Samih Haji Nuhu kwa mkwaju wa penati.

Mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Sofapaka, Januari 20, 2013 na Azam FC kushinda 1-0 kwa bao la mkwaju wa penati la Gaudence Mwaikimba.

Ziara ya Azam FC ilihitimishwa kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya KCB, Januari 22 kwa bao la mkwaju wa adhabu ndogo la Ibrahim Mwaipopo.

Lakini kabla ya ziara hiyo, Azam FC itacheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar, Machi 22, dimbani Azam Complex kuanzia saa moja kamili usiku.