KLABU ya Azam imeendeleza wimbi la kuzoa pointi tatu, baada ya kuishushia dozi ya bao 1-0 Ihefu, katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBC PL).
Azam FC ikiwa nyumbani Azam Complex, ilipata ushindi huo na kufikisha jumla ya pointi 17 baada ya mechi tano, sare mbili na kupoteza mbili, ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.
Mshambuliaji hatari wa kikosi hicho, Prince Dube, ndiye aliyeendeleza makali yake kwa kuifungia bao hilo pekee Azam FC dakika ya 55, akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji Yahya Zayd.
Hilo ni bao la pili mfululizo kwa Dube kwenye mechi mbili zilizopita, baada ya Alhamisi iliyopita kuilaza Simba kwa bao lake sukari, akimtungua kipa Aishi Manula kwa mpira hatari wa kuzungusha.

Muuaji huyo anayetabasamu, amefikisha bao lake la tatu msimu huu kwenye ligi hiyo, akiwa ni miongoni mwa wachezaji wanaowania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora msimu huu.
Benchi jipya la muda la Azam FC, chini ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo, Kocha Mkuu, Kali Ongala na Msaidizi wake, Agrey Moris, linazidi kujiongezea rekodi kwa ushindi mwingine murua, uliowafanya kushinda mechi mbili mfululizo na kutoruhusu wavu kuguswa ‘Cleansheet’.
Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itashuka tena dimbani Novemba 9 mwaka huu, ikiikaribisha Dodoma Jiji, ukiwa ni mchezo wa kiporo.
Kikosi cha Azam FC:
Ali Ahamada, Lusajo Mwaikenda, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Edward Manyama, Isah Ndala/Sospeter Bajana dk 46, Ayoub Lyanga/Idd Nado dk 46, Kenneth Muguna/Yahya Zayd dk 46, Prince Dube/Rodgers Kola, James Akaminko, Kipre Junior/Tape Edinho.