MMILIKI wa klabu ya Azam, Yusuf Bakhresa, leo Jumamosi mchana amekutana na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo na kupata nao chakula cha mchana mara baada ya ushindi muhimu kwenye ‘Mzizima Derby’ dhidi ya Simba.

Mmiliki wa Azam FC, Yusuf Bakhresa, akiongea na wachezaji.

Imekuwa kawaida kwa Bosi Yusuf kuwa karibu na timu, akianzia kwenye zoezi la usajili hadi kwenye mechi za msimu huu, lengo likiwa ni kuwapa hamasa na morali wachezaji.

Bosi Yusuf, ameridhishwa na mwenendo wa timu katika mechi iliyopita baada ya kuifunga Simba bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube, hasa baada yay a wachezaji kuvuja jasho uwanjani kwa kupambania nembo.

“Nawasisitiza wachezaji kupigana na kuipambania jezi ya Azam FC kwenye kila mchezo bila kumdharau mpinzani yoyote, kujitolea na kuheshimu kile mnachoelekezwa na makocha na benchi lote la ufundi,” moja ya kauli ya Bosi Yusuf.

Benchi la ufundi la Azam FC kwa sasa lipo chini ya makocha waliowahi kuichezea Azam FC, kaimu Kocha Mkuu, Kali Ongalla na Agrey Moris, ambaye ni Msaidizi wake.

Wachezaji pia walimwahidi Bosi Yusuf kuwa wataendelea kuzoa pointi tatu katika mechi zijazo, ikiwemo ya Jumatatu dhidi ya Ihefu.

Aidha, katika hatua nyingine, Bosi Yusuf alikabidhiwa zawadi ya jezi ya nyota wa Manchester United, Cristiano Ronaldo, yenye saini yake, aliyopewa na mtaalamu wa tiba za wachezaji wa Azam FC, Mreno Joao Rodrigues kwa niaba yake.

Bosi Yusuf, akikabidhiwa zawadi ya jezi yenye saini ya Ronaldo.

“Nawasihi mashabiki kujitolea na kwenda uwanjani kwa wingi kuwapa moyo wapambanaji wetu, naahidi sapoti yangu na mchango wangu kwenye kila kitu kwa timu hii bora,” alisema Bosi Yusuf