DAKIKA 90 za mchezo wa marudiano wa Azam FC dhidi ya Al Akhdar ya Libya zinakwenda kuitimika kwenye Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumapili saa 1.00 usiku.
Mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika jijini Benghazi, Libya wikiendi iliyopita, Azam FC ilipoteza kwa mabao 3-0.
Katika kuhakikisha inapenya na kusonga mbele, Azam FC imekuja na kauli mbiu ya aina yake iitwayo ‘REMONTADA’, yaani kupindua matokeo ya awali na kuwatoa wapinzani wao hao.
Uongozi wa Azam FC, wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wamejipanga vilivyo, kuhakikisha jambo hilo linatimia.
Wachezaji wa Azam FC wamekuwa na morali kubwa mazoezini, wakihimizana mara kwa mara kufanya vema kwenye mchezo huo kwa kuhakikisha wanapindua meza kibabe.
Si jambo geni Afrika
Katika historia ya soka la Afrika, Azam FC haitakuwa timu ya kwanza kugeuza matokeo na kusonga mbele.
Al Nasr vs Horoya AC (CAF CL, 2018/19)
Moja ya mechi ambazo zimewahi kushtua watu ni ile ya Klabu Bingwa Afrika msimu wa 2018/19, ambapo Horoya AC ya Guinea ilipoteza 3-0 ugenini dhidi ya Al Nasr ya Benghazi.
Lakini ikafanya maajabu kwa kupindua matokeo na kuwatoa Walibya hao kwa jumla ya mabao 6-5, baada ya kuwatandika 6-2 jijini Conakry, Guinea.
Rivers Utd vs El Merreikh (CAF CL, 2016/17)
Miamba ya Sudan, El Merreikh waliwahi kupindua meza kwenye Klabu Bingwa ya Afrika msimu 2016/17, baada ya kupoteza 3-0 ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
Merreikh ilifanya kazi kubwa jijini Khartoum, baada ya kuwatandika Wanigeria hao mabao 4-0 na kusonga mbele kwa raundi ya pili ya michuano hiyo.
Rekodi Azam Complex
Wababe wa Chamazi, Azam FC, wamekuwa na rekodi nzuri ya kuwapiga vigogo wa Afrika kwenye michuano ya Afrika.
Mwaka 2015 kwenye Klabu Bingwa ya Afrika, iliwachapa El Merreikh mabao 2-0 kwenye dimba hilo, mabao ya Azam FC yakiwekwa kimiani na washambuliaji wa zamani, Didier Kavumbagu na John Bocco ‘Adebayor’.
Aidha, wakarudia tena mwaka 2016 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kwa kuwachapa vigogo wa Tunisia, Esperance mabao 2-1, yaliyofungwa na viungo washambuliaji wa zamani, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Farid Mussa.
Hivyo, hakuna kisichowekana jumapili hii, REMONTADA inawezekana, tukutane kwa wingi Azam Complex.
Pambaneni