KLABU ya Azam imeanza vema mwezi Oktoba, baada ya kuichapa Singida Big Stars bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumatatu usiku.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa, Azam FC ikitaka kupata bao la mapema, lakini jitihada zote ziliishia kwenye safu ya ulinzi ya Singida, walioondosha hatari zote.
Kikosi cha Azam FC kilichocheza na Singida Big Stars.
Kwa mara ya kwanza msimu huu tokea akabidhiwe timu, Kocha Mkuu wa Azam FC, Denis Lavagne, alimwanzisha kiungo mshambuliaji, Abdul Sopu, ambaye alionekana kuwa mwiba mchungu kwenye safu ya ulinzi ya Singida hadi alipotoka dakika ya 89.
Dakika ya 17, mshambuliaji Prince Dube, alikaribia kuipatia bao la uongozi Azam FC, baada ya kupiga vema mkwaju wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la 18 na mpira kugonga mwamba wa pembeni kabla ya wachezaji wa Singida kuondosha hatari hiyo.
Kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa, Kipre Junjor, aliendelea na kiwango chake bora baada ya kuichachafya vilivyo safu ya ulinzi ya Singida, kwa staili yake ya kupiga chenga za maudhi huku akishambulia kwa kasi.
Alikuwa ni nahodha wa Azam FC kwenye mchezo huo, Sospeter Bajana, ambaye aliwainua vitini mashabiki wa timu hiyo kwa bao lake safi dakika ya 45, akimtungua kipa wa Singida, Metacha Mnata, kwa shuti kali la mbali baada ya kumegewa pande na James Akaminko.
Bao hilo liliifanya Azam FC kwenda mapumziko kwa uongozi wa bao hilo, ambapo kipindi cha pili, Kocha Mkuu wa Azam FC, Lavagne, alifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumpumzisha Cleophace Mkandala na kuingia Isah Ndala.
Sospeter Bajana, akishangilia bao lake.
Dakika ya 56, Sopu alikaribia kuipatia bao la pili Azam FC baada ya kuipangua safu ya ulinzi ya Singida na kupiga shuti la mbali lililopanguliwa na kipa.
Singida walijitahidi kurejea mchezoni kwa kufanya mashambulizi kadhaa, lakini safu ya ulinzi ya Azam FC ilisimama imara muda wote kuondoa hatari hizo.
Hadi dakika 90 zinamalizika, wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, walifanikiwa kuondoka na pointi zote tatu, ambazo zinaipeleka Azam FC hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 11.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea mazoezini kesho Jumanne jioni kuanza maandalizi kuelekea mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Al Akhdar ya Libya utakaofanyika jijini Benghazi Oktoba 8, mwaka huu.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:
Ali Ahamada, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Daniel Amoah, Edward Manyama, Sospeter Bajana/Ayoub Lyanga (dk 70), Abdul Sopu/Bruce Kangwa (dk 89), Cleophace Mkandala/Isah Ndala (dk 46), Prince Dube/Idris Mbombo (dk 64), James Akaminko, Kipre Junior/Tepsie Evance (dk 64)