KLABU ya Azam imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) baada ya kuishushia dozi nzito Baga Friends ya mabao 6-0.

Hiyo inakuwa mara ya saba mfululizo kwa kikosi cha Azam FC kutinga hatua hiyo, tokea ianze kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza msimu 2015-2016.

Ulikuwa ni usiku mzuri kwa Azam FC, ambayo ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 15 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Charles Zulu, baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Yahya Zayd, akifanya yake dhidi ya Baga Friends.

Mshambuliaji Paul Peter, aliyekuwa kwenye kiwango bora alifunga mabao matatu ya haraka na kukamilisha hat-trick yake katika dakika ya 18, 20 na 44 na kufanya Azam FC kwenda mapumziko ikiwa na uongozi huo mnono.

Mabao mengine ya Azam FC, yaliwekwa kimiani na Paul Katema dakika ya 55 na Daniel Amoah dakika ya 89, yaliyohitimisha ushindi huo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla ya kurejea mazoezini Jumatatu hii, tayari kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya Biashara United, itakayofanyika Uwanja wa Karume, Musoma Februari 23 mwaka huu.