MABINGWA wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC, wametinga hatua ya fainali ya michuano hiyop baada ya kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalty 9-8, mchezo uliomalizika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo Jumatatu jioni.

Mchezo huo ulilazimika kwenda hatua ya penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu, na Azam FC kuibuka kidedea kwenye hatua hiyo kwa kufunga mikwaju yote ya penalti.

Hiyo ni fainali ya sita kwa Azam FC kwenye michuano hiyo, mara zote tano zilizopita ikilitwaa taji hilo, na kufanya kuwa timu pekee iliyolitwaa mara nyingi taji hilo, ikifanya hivyo mara tano.

Katika fainali Azam FC itakutana na Simba, mchezo unaotarajia kufanyika Alhamisi hii saa 2.15 usiku.

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, akipambana na beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.

Azam FC iliuanza vema mchezo huo, ikicheza soka safi na kufanya majaribio kadhaa ya kufunga mabao kipindi cha kwanza, kupitia kwa mshambuliaji Idris Mbombo na Ismail Aziz.

Viungo wa Azam FC, Kenneth Muguna, Frank Domayo, Ibrahim Ajib, walionekana kufanya kazi kubwa ya kudhibiti eneo la kiungo na kupunguza uwezekano wa Yanga kutengeneza nafasi za kufunga mabao.

Safu ya ulinzi ya Azam FC chini ya nahodha Agrey Moris, kipa Mathias Kigonya, beki wa kushoto kinda, Pascal Msindo na wa kulia, Lusajo Mwaikenda, ilifanya kazi kubwa kuokoa hatari zote zilizopelekwa kwenye lango lao.

Wachezaji tisa waliofunga penalti kwa upande wa Azam FC ni Lusajo, Tepsie Evance, Rodgers Kola, Kenneth Muguna, Moris, Daniel Amoah, Yahya Zayd, Paul Katema na Mudathir Yahya, aliyefunga penalti ya ushindi.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Tepsie Evance, akifanya mavitu dhidi ya Yanga.

Mara baada ya mchezo huo, Kamati ya michuano hiyo ilimtangaza kiungo wa Azam FC, Muguna kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo, na kuzawadiwa kitita cha Sh. Milioni 1 kutoka kwa wadhamini Shirika la Bima na Taifa (NIC).

Hiyo ni tuzo ya pili kwa Muguna kwenye michuano hii, ya kwanza akiitwaa wakati Azam FC inaichapa Namungo 1-0 kwenye hatua ya makundi, bao alilofunga yeye.

Aidha pia Azam FC inaandika rekodi ya kuwa timu pekee iliyotwaa tuzo zote za mchezaji bora, wengine waliochukua tuzo hizo ni Frank Domayo ‘Chumvi’ na Mbombo.