MABINGWA wa kihistoria wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC, wanatarajia kushuka dimbani kuivaa Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kesho Jumatatu saa 10.15 jioni.

Azam FC imetinga hatua hiyo baada ya kuongoza Kundi A kufuatia ushindi wa mechi zote tatu za hatua ya makundi, ikizifunga Meli 4 City (1-0), Namungo (1-0) na Yosso Boys (5-1).

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo, wachezaji wakionekana kuwa ari ya kupata matokeo mazuri kwa kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali na kuchukua taji hilo kwa mara ya sita.

Wachezaji wa Azam FC wanaotarajia kukosekana kwenye mchezo huo ni kipa Ahmed Salula, mabeki Nickolas Wadada, Abdallah Kheri, mshambuliaji Shaaban Chilunda, ambao ni majeruhi.

Kipa wa Azam FC, Zuberi Foba, akiokoa mchomo wa Lusajo Mwaikenda mazoezini.

Rekodi

Hii itakuwa ni mara ya sita kwa Azam FC kukutana na Yanga kwenye michuano hiyo, wababe hao wa Chamazi wakiwa na rekodi nzuri, wakiifunga mechi tatu, wakipoteza mbili na moja ikiisha kwa sare.

Mwaka jana kwenye michuano iliyopita, Azam FC ilikutana na Yanga kwenye hatua hiyo, na kushuhudiwa dakika 90 zikiisha kwa sare ya bao 1-1, Yanga ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-4.

Rekodi ya mabao mengi ambayo inasimama hadi sasa kwenye mechi hizo sita, ni Azam FC kuichabanga Yanga mabao 4-0 mwaka 2017, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, Joseph Mahundi, Yahya Mohammed na Enock Atta.