KLABU ya Azam FC imekamilisha hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kishindo baada ya kuichapa Yosso Boys mabao 5-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo Jumamosi jioni.

Ushindi huo unafaifanya Azam FC kukata tiketi ya kukutana na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, mchezo utakofanyika Uwanja wa Amaan keshokutwa Jumatatu saa 10.15 jioni.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Azam FC kwenye michuano hiyo, ikifanikiwa kushika uongozi wa Kundi ikivuna pointi tisa, ikifuatiwa na Namungo aliyejikusanyia sita, Meli 4 City ikiwa nazo tatu huku Yosso wakiwa hawana pointi yoyote.

Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo, yalifungwa na mshambuliaji Idris Mbombo, aliyefunga mawili dakika ya 40 kwa mkwaju wa penalti kufuatia kuangushwa ndani ya eneo la hatari na lingine akitupia dakika ya 66 akiunganisha krosi ya Edward Manyama.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Ismail Aziz, akipambana na beki wa Yosso Boys.

Beki Daniel Amoah, alitupia bao jingine dakika ya 52 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Manyama, huku Ismail Aziz, aliyekuwa kwenye kiwango bora akipiga la nne baada ya kumzidi maarifa beki wa Yosso na kupiga shuti lililomshinda kipa.

Yosso Boys walijifunga wenyewe kupitia kwa Dau, likiwa ni bao la tano kwa Azam FC dakika ya 74, lililotokana na krosi ya Mbombo kuguswa na Ismail kabla ya kumkuta Dau aliyejifunga kwenye harakati za kuokoa mchomo huo.

Mechi zote wachezaji bora

Mara baada ya mchezo huo, Kamati ya michuano hiyo ilimtangaza mshambuliaji wetu, Mbombo kuwa Mchezaji Bora wa mechi hiyo na kuzawadiwa kitita cha Sh. 500,000 na wadhamini Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, akikabidhiwa zawadi yake ya kuwa Mchezaji Bora wa mechi.

Hiyo inafanya Azam FC kuandika rekodi ya kuwa timu pekee iliyotoa wachezaji bora kwenye mechi zote walizocheza kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mechi ya kwanza dhidi ya Meli 4 City alikuwa Frank Domayo ‘Chumvi’, mechi ya pili tulipoichapa Namungo bao 1-0 alichaguliwa Kenneth Muguna, huku hii ya mwisho akiwa Mbombo.