MARA baada ya kutinga hatua ya nusu fainali, kikosi cha Azam FC kinatarajia kumalizia hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kukipiga dhidi ya Yosso Boys kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.

Azam FC ipo Kundi A, ikiwa imeshinda mechi zake zote mbili za awali ikijikusanyia jumla ya pointi sita sawa na Namungo, baada ya kuzichapa Meli 4 City na Namungo, zote kila moja kwa ushindi wa bao 1-0.

Wachezaji wa Azam FC wakiwa mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Yosso Boys.

Kikosi hicho kimeonekana kuimarika kiuchezaji kadiri siku zinavyokwenda, wachezaji wakiufurahia mpira kwa pasi fupi fupi wakiwa chini ya Kocha wa muda, Abdihamid Moallin.

Ubora wa kiuchezaji umeifanya Azam FC kutoa wachezaji bora kwenye mechi zote mbili ilizocheza, mechi ya kwanza dhidi ya Meli 4 akiwa nahodha msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi na ile ya jana iliyocheza na Namungo, akichaguliwa Kenneth Muguna.

Wachezaji wote hao walizawadiwa kitita cha Sh. 500,000 kila mmoja kama zawadi kutoka kwa Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Kocha wa muda wa Azam FC, Abdihamid Moallin, akitoa maelekezo mazoezini.

Aidha Azam FC ambayo ndiyo mabgingwa wa kihostoria wa michuano hiyo, itawakosa wachezaji wake wawili kwenye mchezo huo, beki Nickolas Wadada na mshambuliaji Yahya Zayd, ambao ni majeruhi.

Ushindi wowote au sare kwa Azam FC utaifanya kukutana na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, ikishika nafasi ya pili itakutana na Simba kwenye hatua hiyo.