TUTATUMIA vema uwanja wa nyumbani! Hivyo ndivyo ilivyojipanga Klabu ya Azam kufanya vema kwenye mchezo wa kesho Jumanne dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) utafanyika Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1.00 usiku, Azam FC ikijipanga kuvuna pointi zote tatu kwenye kipute hicho.

Kiungo wa Azam FC, Khleffin Hamdoun, akiwa mazoezini huku mvua ikinyesha leo Jumatatu.

Wachezaji wa Azam FC wana ari kubwa kuelekea mchezo huo, wakitaka kuondoa matokeo mabaya ya mechi iliyopita dhidi ya KMC ilipopoteza ugenini 2-1.

Hakuna majeruhi yoyote mpya kwenye kikosi cha Azam FC, ambapo mchezaji pekee atakayekosekana ni mshambuliaji Prince Dube, anayeendelea na programu maalumu ya mazoezi ya kurejea dimbani.

Azam FC hadi sasa imeshacheza mechi sita za ligi, ikifanikiwa kushinda mbili, sare moja, na kupoteza mechi tatu, zote zikiwa za ugenini.

Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi, haijashinda mchezo wowote ikiwa imepoteza mechi nne na kutoka sare mbili.

Takwimu.

Kihistoria tokea Azam FC ipande Ligi Kuu mwaka 2008, imekutana mara 26 na Mtibwa Sugar kwenye mechi za ligi, ikishinda mara 12, sare tisa na kupoteza tano.

Azam FC ikiwa na rekodi nzuri dhidi ya Mtibwa Sugar, mara zote zilipokutana kwenye ligi.

Mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014, wana wastani mzuri wa kufunga mabao ikiwa inacheza na Mtibwa Sugar, katika mechi hizo zote ikiwa imeziona nyavu za wapinzani wake hao mara 33, huku Mtibwa ikitupia 18.

Rekodi hiyo inaonyesha kuwa, Azam FC haijawahi kupoteza mchezo wowote wa ligi inapocheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex.