KLABU ya Azam FC imeinyuka JKU mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumamosi jioni.

Mchezo huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji wa kikosi hicho wakati huu wa mapumziko ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) kupisha mechi za timu za Taifa.

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, akifunga moja ya mabao yake.

Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo yaliwekwa kimiani na mshambuliaji Idris Mbombo, aliyefunga mawili, la kwa akitupia kwa mkwaju wa penalti dakika ya 19 baada ya kuangushwa ndani ya eneo la 18, jingine aliweka kimiani dakika ya 41, akimalizia kazi nzuri ya Ismail Aziz.

Nyota kutoka Zambia, Charles Zulu na Rodgers Kola, walitupia mengine na kuhitimisha ushindi huo mnono wa Azam FC kwa mabao mawili safi, dakika ya 23 na 89.

Winga wa Azam FC, Charles Zulu, akishangilia bao lake na Mbombo.

Azam FC ilipata pigo kwenye mchezo huo, kwa nahodha wake Sospeter Bajana, kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 80 na kulazimika kucheza pungufu kwa wachezaji wawili baada ya awali Zulu kuuumia na nafasi yake kukosa mtu wa kuingia kutokana na benchini kutokuwa na mchezaji wa kuingia.

Benchi la ufundi la Azam FC liliutumia mchezo huo pia kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo ujao wa ligi dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Uhuru Novemba 21, mwaka huu saa 10.00 jioni.