KIKOSI cha Azam FC tayari kimeanza maandalizi kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Novemba 20, mwaka huu.

Wachezaji wa Azam FC wanaendelea kujifua kwa siku ya tatu leo Jumatano, wakijiandaa vilivyo ili kufanya vema katika mchezo huo muhimu.

Nyota pekee wanaokosekana mazoezini ni wale sita walioripoti timu za Taifa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.

Wachezaji wa Azam FC, kutoka kushoto Charles Zulu, Khleffin Hamdoun na Ismail Aziz, wakiwa kwenye programu ya mazoezi.

Walioko timu za Taifa ni kipa Mathias Kigonya (Uganda), Nahodha Msaidizi, Bruce Kangwa (Zimbabwe), kiungo Kenneth Muguna (Kenya) huku watatu wakiwa Taifa Stars, ambao ni mabeki Lusajo Mwaikenda, Edward Manyama na winga Idd Seleman ‘Nado’.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema kuwa kitu kikubwa wanachokiangalia ni kutengeneza utimamu wa mwili kwa wachezaji kwa siku mbili za mwanzo (Jumatatu na Jumanne) kabla ya kuhamia kwenye ufundi.

Beki wa Azam FC, Daniel Amoah, akimiliki mpira dhidi ya Rodgers Kola, mazoezini wiki hii.

“Tunatakiwa kuandaa mechi na KMC tutaiandaa kwa kila kitu kinachohitajika kwenye ulinzi kwenye ufundi na nguvu,” alisema.

Ili kujiandaa vema na mchezo huo, benchi la ufundi limepanga kucheza mechi moja ya kirafiki ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji wikiendi hii.