KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Tepsie Evance, ameweka wazi kuwa shukrani ziende kwa benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha kwenye mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold.

Azam FC imekipiga na timu hiyo kwenye mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji Rodgers Kola, aliyemalizia krosi ya Tepsie.

Tepsie aliingia dakika 15 za mwisho, ikiwa ndio mechi yake ya kwanza msimu huu, akichukua nafasi ya Ayoub Lyanga, ambapo mbali na kutoa pasi ya mwisho ya bao, kiungo huyo aliwaweka kwenye wakati mgumu wachezaji wa Geita Gold kwa muda mchache tu aliocheza.

Kiungo wa Azam FC, Tepsie Evance, akifanya yake dhidi ya Geita Gold.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Tepsie alisema benchi la ufundi linahitaji kupewa shukrani kwani kwa muda mrefu tokea kipindi cha maandalizi ya msimu, wameonyesha kumwamini.

“Wameonyesha kuniamini toka kwenye maandalizi ya msimu na kwenye mechi za ligi nikiwa sehemu ya mchezo lakini nakuwa sipati nafasi lakini leo (jana) wameniamini wamenipa maelekezo niliyoyafanya ndio waliyonielekeza na tumeweza kupata ushindi,” alisema.

Kiungo huyo chipukizi ni mmoja wa wachezaji waliokulia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’, msimu uliopita akicheza kwa mara ya kwenye ligi baada ya kutolewa kwa mkopo Ihefu kabla ya msimu huu kuaminiwa na kuwa sehemu ya wachezaji waliobakishwa kwa ajili ya kikosi hiki.