BAO pekee lililofungwa na mshambuliaji Rodgers Kola, limeihakikishia pointi tatu muhimu Azam FC, ikiichapa Geita Gold bao 1-0.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL), ulifanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex leo Jumanne usiku, vijana wa Azam FC wakitakata vilivyo kwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani.

Mshambuliaji, Rodgers Kola, akishangilia bao lake dhidi ya Geita Gold.

Kola alitumia dakika 14 tu tokea aingie uwanjani dakika ya 67 kuchukua nafasi ya kiungo mshambuliaji, Kenneth Muguna, kuweza kuipatia bao hilo Azam FC, akitumia vema pasi ya pembeni ya kiungo Tepsie Evance.

Hilo linakuwa bao la kwanza la mashindano kwa Kola kuifungia Azam FC tokea ajiunge nayo msimu huu, akiwa amecheza mechi tatu pekee za ligi, moja akianza (vs Namungo) na mbili akiingia kutokea benchi.

Kuingia kwa Kola na baadaye Tepsie kipindi cha pili, kwa kiasi fulani kuliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC, mshambuliaji huyo akifanikiwa kuishinda mipira yote ya juu huku kiungo huyo akipeleka hatari nyingi langoni mwa Geita Gold.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akichuana na kiungo wa geita Gold, Kevin Nashon.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi saba kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nafasi ya saba ikizidiwa pointi nane na kinara Yanga, aliyefikisha pointi 15.

Mara baada ya mchezo huo, ligi hiyo inatarajiwa kuwa mapumzikoni kwa wiki takribani tatu kupisha mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar, ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’ itamalizia mechi zake mbili za makundi dhidi ya Congo DR na Madagascar.

Ligi hiyo itaendelea tena Novemba 21 mwaka huu, Azam FC tukikipiga dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, saa 10.00 jioni.