KWA mara ya kwanza baada ya miaka minne, Klabu ya Azam FC imepoteza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa usiku huu, ikifungwa mabao 2-0.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Yanga kwenye uwanja huo, ilikuwa ni Aprili Mosi, 2017, ukiwa ni msimu wa 2016/2017.

Mchezo huo ulianza kwa kasi timu zote zikishambuliana kwa zamu, Azam FC ikiwatumia viungo wake washambuliaji wa pembeni, Idd Seleman ‘Nado’ na Never Tigere, kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga.

Kiungo wa Azam FC, Kenneth Muguna, akimiliki mpira mbele ya kiungo wa Yanga, Yannick Bangala.

Dakika ya 15, pasi ya juu iliyopigwa na kiungo wa Azam FC, Kenneth Muguna, ilipita juu kidogo ya mshambuliaji Rodgers Kola na mpira kutoka nje ya lango.

Dakika ya 33, kama mwamuzi wa mchezo huo, Heri Sasi, angekuwa makini kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka, angeweza kuipatia mkwaju wa penalti Azam FC, baada ya beki wa Yanga, Dickson Job, kumwangusha ndani ya eneo la hatari Nado, lakini mwamuzi alikataa.

Tukio ambalo lingeinufaisha Azam FC kupata mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Yanga, Dickson Job, kumsukuma winga wa Azam FC, Idd Seleman .Nado’.

Kosa kosa nyingine ya Azam FC ilikuwa ni dakika ya 42, ambapo mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na beki wa kushoto, Edward Manyama, ulimkuta beki Daniel Amoah, aliyepiga kichwa kilichopanguliwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo yalifungwa na Fiston Mayele dakika ya 36 na Jesus Moloko dakika ya 73, yaliyowafanya kuondoka na ushindi huo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kusalia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza mara mbili.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuumana dhidi ya Geita Gold kwenye mwendelezo wa ligi hiyo, ukifanyika Uwanja wa Azam Complex Jumanne ijayo saa 2.30 usiku.