“TUNAJUA tunaenda kutafuta nini” Hiyo ndio kauli ya benchi la ufundi la Azam FC kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya Yanga utakaofanyika Uwanja wa Mkapa, kesho Jumamosi saa 1.00 usiku.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati ameweka wazi kuwa wanahitaji pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo licha ya kukiri wanacheza na timu ambayo si nyepesi kutokana na nafasi ya juu waliyopo katika msimamo wa ligi.

“Tunajua tunacheza na timu ambayo sio nyepesi, kwenye msimamo wa ligi muda huu ipo juu, sisi tunajua tutacheza mchezo gani, tunajua tumepanga nini na tunajua tunaenda kutafuta nini,” alisema Bahati.

Morali ipo juu

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye hali nzuri kabisa na morali ikiwa juu kuelekea mchezo huo, Kocha Bahati akieleza kuwa kila mchezaji anaitamani mechi hiyo kutokana na ari wanayoionyesha wakiwa mazoezini.

Ari ipo juu kikosini, angalia mtifuano wa viungo Frank Domayo ‘Chumvi’ na Kenneth Muguna, mazoezini.

Wachezaji wa Azam FC hadi wanamaliza mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo leo Ijumaa asubuhi, kikosini hamna majeruhi yoyote hali inayoonyesha kuwa nyota wote wapo tayari kabisa kwa kipute hicho kinachosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka.

Msimamo wa ligi

Wakati Azam FC ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi nne kwenye nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi moja, kutoka sare moja na kupoteza moja, Yanga yenyewe ipo kileleni sawa na Polisi Tanzania, ikiwa na pointi tisa ikishinda mechi zote tatu za mwanzo.

Azam FC itaingia dimbani ikitaka kusaka ushindi muhimu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi kwa kupunguza pengo la pointi baina yake na waliokuwa juu katika msimamo.

Takwimu muhimu

Wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, wamekuwa na matumizi mazuri ya Uwanja wa Mkapa kila inapocheza na Yanga, ambapo itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbumbuku ya ushindi wa bao 1-0 zilipokutana mara ya mwisho, bao pekee likifungwa na mshambuliaji nyota, Prince Dube, kwa shuti zuri la mbali.

Moja ya makipa bora kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL), Mathias Kigonya, akiwa mazoezini

Katika mechi tano zilizopita za Azam FC dhidi ya Yanga zilipokutana kwenye ligi ndani ya dimba hilo, Matajiri hao wa Azam Complex wameshinda nne kati ya hizo na mchezo mmoja ukiisha kwa suluhu.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza ikicheza na Yanga kwenye uwanja huo ni Aprili Mosi, 2017, mchezo ulioisha kwa ushindi wa Wanajangwani hao wa bao 1-0.

Timu hizo zimekutana kwenye jumla ya mechi 26 za ligi, zikilingana katika takwimu za ushindi, kila mmoja akishinda mara tisa dhidi ya mwenzake huku zikipatikana sare nane.

Aidha Azam FC inaongoza kufunga bao moja dhidi ya Yanga kwenye jumla ya mabao 59 yaliyofungwa katika mechi zote, Azam FC ikiziona nyavu za mpinzani wake huyo mara 30 na Yanga ikifanya hivyo mara 29.

Mshambuliaji, Idris Mbombo, alifunga bao muhimu lililoipa Azam FC ushindi, kwenye mchezo wa mwisho wa NBCPL dhidi ya Namungo.

Nahodha wa zamani wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, hadi sasa anabakia kwenye historia ya timu hiyo kwani ndiye kinara wa kuziona nyavu za Yanga kila alipokutana nao kabla hajaondoka, akiwa ameziona nyavu zao mara 10.

Wachezaji wengine kwenye historia ya Azam FC wanaofuatia ni washambuliaji, Kipre Tchetche, Shaaban Chilunda na Yahya Tumbo, ambao kila mmoja ametupia kambani katika nyavu za Yanga mara mbili.