BEKI wa kati chipukizi wa Klabu ya Azam, Lusajo Mwaikenda, ameweka wazi yupo tayario kucheza popote atakapopangwa kikosini kwenye mechi.

Kauli ya beki huyo imekuja siku chache mara baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, kumbadilisha namba kwa kumchezesha kama beki wa kulia katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Namungo na Pyramids.

Lusajo ameonekana kufanya vema katika nafasi hiyo, jambo ambalo linaendelea kulishawishi benchi la ufundi kumtumia zaidi beki huyo, ambaye kiwango chake kinapanda kwa kasi kubwa.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz,  Lusajo alisema kuwa popote pale mwalimu atakapotaka acheze anaweza kucheza kwa kufuata maelekezo anayopewa.

“Hii yote ni kwa sababu ya mwalimu na maelekezo anayonipa kuwa ananichezesha nafasi ambayo si yangu lakini nakupa majukumu Fulani moja mbili tatu nenda kayatekeleze,” alisema.

Beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda, akimtoka kiungo mshambuliaji wa Pyramids ya Misri, Ramadan Sobhi.

Aliongeza kuwa; “Mimi nadhani mwalimu ndio anajua anitumie wapi, beki wa kati, beki wa kushoto au kulia, kokote ananipanga mwalimu, mimi popote pale naweza kucheza endapo mwalimu atataka nicheze kwa majukumu yake atakayonipa niko radhi kwenda kuyatekeleza.”

Kocha amsifia

Kiwango chake bora kimelivutia benchi la ufundi la Azam FC, baada ya Kocha Msaidizi, Vivier Bahati, kusema kuwa wamefurahishwa na ubora aliouonyesha Lusajo kwenye mechi hizo.

“Lusajo ameonyesha kiwango bora sana sisi kama benchi la ufundi tumefurahishwa sana, alianza kucheza vema mechi na Namungo kwenye nafasi tofauti tuliyompanga lakini kitu kizuri zaidi akacheza kwa ubora zaidi katika mechi dhidi ya Pyramids.

“Ni mchezaji kijana anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi, ametuonyesha kitu kikubwa sana, anacheza vema mipira ya juu, kuzuia chini na anatumia akili sana, lakini kikubwa zaidi ni mchezaji mwenye nidhamu kubwa, kila maelekezo tunayompa amekuwa akitekeleza, hii inatoa changamoto kwa watu wanaowania nafasi hiyo kupambana zaidi yake,” alisema Bahati.

Kikosi cha Azam FC leo Jumanne kinatarajia kuanza maandalizi kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Mkapa Jumamosi hii saa 1.00 usiku.