KIKOSI cha Azam FC kimerejea salama leo Jumatatu mchana kikitokea jijini Cairo, Misri kilipoenda kucheza dhidi ya Pyramids.

Mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika uliisha kwa Azam FC kupoteza kwa bao 1-0, na hivyo kutolewa kwa ushindi wa jumla wa 1-0 kufuatia suluhu kwenye mchezo wa awali uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Wachezaji wawili wa Azam FC, Abdallah Kheri (kutoka kulia) na Khlefin Hamdoun, walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Licha ya Azam FC kutolewa, wachezaji wa timu hiyo walionyesha mchezo mzuri kwa kucheza kwa nudhamu kubwa na kupambana kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Mara baada ya kikosi hicho kuwasili, wachezaji wamepewa mapumziko ya siku moja hadi kesho Jumanne saa 1.00 usiku watakapoanza maandalizi kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara (NBCPL) dhidi ya Yanga.

Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Omary Kuwe (kushoto) na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira, Dr. Jonas Tiboroha, walipowasili.

Mtanange huo utafanyika Uwanja wa Mkapa Jumamosi hii saa 1.00 usiku.