KLABU ya Azam FC, imetoka suluhu dhidi ya Pyramids ya Misri katika mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumamosi saa 9.00 Alasiri.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuhitaji sare yoyote ya mabao au ushindi, kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika jijini Cairo, Misri Oktoba 24 mwaka huu.

Mchezo huo ulianza kwa kasi, ikipoteza nafasi nzuri ya kuandika bao la uongozi katika dakika 15 kupitia kwa mshambuliaji Idris Mbombo, aliyepiga shuti lililomlenga kipa baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa kiungo mshambuliaji Idd Seleman ‘Nado’.

Dakika chache baadaye almanusura Azam FC iandike bao la uongozi, baada ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo mshambuliaji, Never Tigere, kupanguliwa na kipa wa Pyramids na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Never Tigere, akimtoka mchezaji wa Pyramids ya Misri.

Safu ya ulinzi ya Azam FC chini ya mabeki wa kati, Daniel Amoah na Abdallah Kheri, ilionekana kusimama imara kwa muda wote wa mchezo, wakifanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi yote ya wapinzani wao.

Uimara wao ulichagizwa na uwepo wa safu ngumu ya kiungo wa ukabaji juu yao, ambayo iliundwa na wachezaji wawili, Sospeter Bajana na Paul Katema, ambao walifanya kazi kubwa ya kuilinda safu ya ulinzi isifikiwe kirahisi.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuhitaji sare yoyote ya mabao au ushindi, kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika jijini Cairo, Misri Oktoba 24 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kushuka tena dimbani Jumanne ijayo, kikicheza dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, utakaofanyika Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.