KLABU ya Azam FC inatarajia kujitupa uwanjani kuivaa Pyramids ya Misri katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumamosi saa 9.00 Alasiri.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuiondosha mashindanoni, Horseed ya Somalia kwa jumla ya mabao 4-1, katika raundi ya awali ya michuano hiyo.

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, akipambana na nahodha wa Horseed ya Somalia, timu hizo zilipokutana kwenye raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Azam FC kipo vizuri kabisa kuelekea mchezo huo wa kwanza, wachezaji wakiwa na morali ya hali ya juu kuhakikisha wanapata matokeo bora katika mchezo huo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri pale watakaporudiana baada ya wiki moja.

Mchezaji pekee wa Azam FC, ambaye atakosekana kwenye mchezo huo ni mshambuliaji Prince Dube, ambaye anaendelea na programu ya mazoezi mepesi tayari kurejea dimbani.

Kocha anena

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, alisema kuwa wachezaji wote wapo vizuri tayari kusaka matokeo mazuri.

“Kila mtu yupo vizuri tunawaamini watu wote kila atakayepata nafasi nina imani atajitoa kwa kiwango kikubwa, tutawaheshimu Pyramids ila kwa uwanjani kesho dakika tisini nina imani tutatoa uwezo wetu mkubwa kila mtu atajitoa mia kwa mia,” alisema.

Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina, akitoa maelekezo kwa wachezaji wake

Kocha huyo aliongeza kuwa, ana Imani wachezaji wa kikosi hicho watafanya kitu kikubwa kwenye mchezo huo kitakachowapatia matokeo mazuri.

Nahodha afunguka

Naye nahodha msaidizi wa Azam FC, Sospeter Bajana, ameeleza kuwa wamepata muda mrefu wa maandalizi kuelekea mtanange huo, huku akiwaahidi mashabiki matokeo mazuri.

“Mimi niko vizuri pamoja na wachezaji wenzangu, tumepata muda mzuri sana wa kujiandaa na mechi hii na tumekaa na walimu wetu wametuelekeza namna ya kufanya na namna ya kwenda kucheza mechi hiyo kwa hiyo naamini kila kitu kiko sawa,” alisema.

Mashabiki 2,000 ruksa

Baada ya kushindwa kuingiza mashabiki wetu kwenye mechi zetu mbili zilizopita za mashindano hayo, hatimaye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeturuhusu kuingiza mashabiki wasiozidi 2,000 katika mchezo huo.

Mashabiki 2,000, waruhusiwa kuingia uwanjani kwenye mchezo huo.

CAF walikuwa wakizuia mashabiki kwenye mechi za mashindano hayo ili kupambana na changamoto za ugonjwa wa Uviko-19, ambao umeitikisa dunia tangu Machi, mwaka jana.

Big Screen kama kawaida

Katika kuonyesha tunawajali mashabiki wetu, Azam FC tutafunga luninga kubwa (big screen) kwa kushirikiana na Kampuni ya Natkern, itakayowawezesha mashabiki mbalimbali kushuhudia mchezo huo kwa kiwango cha hali ya juu.

Luninga hiyo, tutaifunga kwenye eneo la ndani geti namba moja ndani ya viunga vya Azam Complex.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Tepsie Evance, akifanya yake kwenye mazoezi ya mwisho leo Ijumaa asubuhi.

Mara baada ya mchezo huo wa kwanza, timu hizo zinatarajia kurudiana Oktoba 24 mwaka huu jijini Cairo, Misri na mshindi wa jumla atasonga mbele kwa raundi ya mwisho ya mtoano (play off), akikutana na moja ya timu iliyotoka katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.