KLABU ya Azam FC tumeingia makubaliano na Kampuni ya Natkern Limited kwa ajili ya kufunga luninga kubwa (LED Screen) kwa ajili ya mashabiki kuangalia mchezo wao dhidi ya Pyramids ya Misri Jumamosi hii.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, utaanza saa 9.00 Alasiri kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC imeamua kufunga luninga hiyo, ili kuwapa fursa mashabiki wa soka kushuhudia mchezo huo kwa pamoja kutokana na katazo la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambalo limeendelea kusimamia msimamo wake wa kutohitaji mashabiki kuingia uwanjani.

Meneja Masoko na Mauzo wa Azam FC, Tunga Ally (wa pili kutoka kushoto), akiwa sambamba na Maofisa wa Kampuni ya Natkern kukagua sehemu itakapofungwa luninga kubwa.

Luninga hiyo ya kisasa kabisa itafungwa na Kampuni ya Natkern, kwenye geti namba moja la Azam FC upande wa kantini, ambako ndipo mashabiki wataingia kushuhudia mchezo huo.

Mbali na kushushudia mchezo huo, pia vitakuwepo vinywaji mbalimbali vyenye viwango vya hali ya juu kutoka chapa namba moja ya Makampuni ya Bakhresa (SSB), kama vile Azam Energy, Ukwaju, Maji ya Uhai, African Fruti, Azam Cola, Mango Crush, Apple Punch.

Aidha kutakuwa pia na burudani mbalimbali za michezo ya watoto, ambao watafurahi pamoja kwa kucheza kwenye bembea za kisasa zaidi.

Natkern ni kampuni inayojihusisha na ufungaji na ukarabati wa LED Screen za aina zote za kibiashara pamoja na za matukio mbalimbali (events).