BASI jipya la klabu ya Azam FC, Mercedes Benz Irizar i6S Plus, limeendelea kuzua gumzo nchini na kwenye anga za kimataifa kutokana na ubora wake mkubwa.

Basi hilo lenye hadhi kubwa ya kimataifa linalotumiwa pia na baadhi ya timu kubwa duniani, Liverpool FC na Real Madrid, tayari limewashawasili jijini Dar es Salaam juzi Jumapili usiku.

Mercedes Benz Irizar i6S Plus, ikiwa mjini Tunduma, Somgwe.

Azam FC inakuwa timu ya kwanza Tanzania na sehemu kubwa Afrika, kumiliki basi la kifahari la hadhi hiyo, ambalo limepachikwa jina la ndege ya ardhini kutokana na hadhi yake nje na ndani.

Limewasili nchini likipita barabara kwa barabara kutokea jijini Gauteng, Afrika Kusini hadi jijini Dar es Salaam, likipita nchi nne tofauti za Afrika, ambazo ni Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe na Zambia.

Popote lilipopita katika nchi hizo, basi hilo lilikuwa kivutio kikubwa kwa watu mbalimbali, ambao walikuwa wakipiga nalo picha, wengine wakienda mbali zaidi wakitaka kuona muonekano wake wa ndani.

Wakati basi likiwa mjini Tunduma, Songwe, Azam FC iliweza kuweka jiwe la msingi na ujenzi wa tawi la mashabiki wa mji huo linaloitwa Sogea, lenye mamia ya mashabiki.

Meneja Masoko na Mauzo wa Azam FC, Tunga Ally, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa tawi la Sogea, mjini Tunduma, Songwe.

Baadhi ya mikoa ambayo basi hilo limepita kabla ya kuwasili Dar es Salaam, mara baada ya kuingia mpakani mwa Zambia na Tanzania, Tunduma, ni Songwe, Mbeya, Iringa na Morogoro.

Wakazi wa mikoa hiyo walikuwa wakilifurahia, na kulisimamisha basi hilo kila walipoliona barabarani, jambo ambalo limekuwa kivutio kikubwa na picha kusambaa kwa kasi kubwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Rais Mh. Samia Suluhu, tuko pamoja nawe, Kazi Iendelee!

Mitandao mbalimbali ya kimataifa kama vile ‘African Soccer Updates’, nayo imepongeza kitendo cha Azam FC kutembeza basi hilo barabara kwa barabara, wakidai ni njia nzuri ya kujitangaza.

Mtandao huo (African Soccer Updates) kwenye andiko lake la Alhamisi iliyopita kwa tafsiri ya lugha ya kiswahili, iliandika kuwa: “Kama jambo hili limefanyika bila kupangwa au kama limepangwa, Azam kuamua kuendesha basi lao kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania litabakia kuwa mojawapo ya mambo ya kibunifu sana ya kujitangaza kama chapa katika siku za hivi karibuni. Katika siku 4-5 zilizopita basi hili limeonekana katika nchi 4 tofauti za ukanda wa COSAFA.”

Azam FC ambayo imekuwa na programu mbalimbali za mashule, Wakati basi hilo likiwa mkoani Mbeya, liliweza kupitishwa kwenye Shule ya Msingi na Sekondari ya Vanessa, ambapo wanafunzi waliweza kulipokea kwa staili ya aina ya kulipigia makofi wakilizunguka pande zote basi hilo na kuimba kauli mbiu ya Azam FC “Timu Bora, Bidhaa Bora”.

Wanafunzi wa Sekondari ya Meta, jijini Mbeya wakifanya yao.

Vilevile liliweza kupita kwenye Sekondari ya Meta, nako likipokelewa vema na wanafunzi wa shule hiyo.

Bondia mahiri nchini, Twaha Kiduku, aliwoangoza wakazi wa mji wa Morogoro, kulipokea basi la Azam FC kwa staili ya aina yake, jambo ambalo lilileta amshaamsha kuanzia kwenye saluni yake ya Kiduku Barbershop hadi Stendi Kuu ya Msamvu, alipomalizia zoezi hilo.

Bondia mahiri nchini, Twaha Kiduku, akilipokea basi la Azam FC kwa staili ya aina yake.

Popote Basi lililopita nchini, kuanzia Tunduma, Azam FC kupitia Meneja Mauzo na Masoko, Tunga Ally, imeuza jezi nyingi kwa mashabiki wengi wa soka jambo ambalo limeiingizia timu kipato na kuitangaza chapa ya timu pamoja na Makampuni ya Bakhresa Group (SSB) kwa ujumla.

Kwa ajili ya kuogezewa muonekano mpya wa ndani, basi hilo litapelekwa kwa wataalamu wa kazi hiyo, Kampuni ya Azam Upholstery Co Ltd, iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambayo ndio kampuni pekee inayolipa gari yako muonekano mpya wa ndani na nje kwa hadhi ya kimataifa, ikiwa imefanya kazi nyingi za ndani na nje ya nchi kwa kiwango cha hali ya juu.

Mercedes Benz Irizar i6S Plus ikiwa imepaki kwa mabingwa wa kuupa muonekano mpya wa ndani na nje wa gari yako, Azam Upholstery Co Ltd.

Hiyo ni historia nyingine ambayo Azam FC inazidi kuiandika, ikiwa inajijenga msimu hadi msimu kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa, na hilo ni basi lake la pili la kifahari baada ya lile awali ambalo ilikuwa ikilitumia la Higer.