Uongozi wa Azam Football Club unathibitisha kwamba umewasimamisha wachezaji watatu waandamizi kwa muda usio na ukomo ndani ya msimu huu wa 2021/22.

Wachezaji hao ni nahodha mkuu Aggrey Morris, na wasaidizi wake, Salum Abubakar na Mudathir Yahya.

Sababu ya hatua hii ni utovu wao wa nidhamu dhidi ya meneja wa timu, Luckson Kakolaki, Septemba 18, 2021, siku ya mchezo wa pili wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed SC ya Somalia.

Kabla ya mchezo walimfuata ofisini kwake na kumtamkia maneno yasiyo na staha, na baada ya mchezo wakarudia tena mbele ya wachezaji wenzao, benchi la ufundi na viongozi wote wa klabu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Taratibu za kinidhamu zilifuatwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia nafasi ya kusikilizwa mbele ya kamati ya nidhamu ya klabu.

Lakini maelezo yao ya utetezi yalikosa mashiko mbele ya kamati hiyo na ndiyo maana adhabu hii inachukuliwa.

Azam FC inasimamia misingi ya weledi ikiwemo nidhamu ikiamini ndiyo njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio endelevu.

 IMETOLEWA NA

MKUU WA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO AZAM FC,

THABITH ZAKARIA,

OKTOBA 06, 2021