KLABU ya Azam FC imeshindwa kutamba ugenini, baada ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika jana Jumamosi jioni, umepigwa kwenye Uwanja wa Ushirika, jijini Moshi, Kilimanjaro.

Huo ni mchezo wa kwanza kihistoria, Azam FC inapoteza dhidi ya Polisi Tanzania, kwani kwenye mechi nne zilizopita, Wababe hao wa Azam Complex wameshinda zote bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Azam FC ndio ya kwanza kupata nafasi ya kuandika bao la uongozi ndani ya dakika 10 za mwanzo za mchezo huo, kupitia kwa mshambuliaji Idris Mbombo.

Nafasi ya kwanza ya kufunga kwa Azam FC, iliyopotezwa na Idris Mbombo.

Mbombo, aliunasa mpira uliookolewa vibaya na mabeki akiwa ndani ya eneo la 18, lakini shuti alilopiga lilipanguliwa na kipa wa Polisi Tanzania, Metacha Mnata, kabla ya mabeki kuondosha hatari hiyo.

Wenyeji walijipatia bao la uongozi dakika ya 23, lilifungwa na Kassim Shaban, aliyeunasa mpira uliopanguliwa na kipa wa Azam FC, Mathias Kigonya.

Dakika sita baadaye mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo mkabaji, Sospeter Bajana, ulitumiwa vema na kiungo Idd Seleman ‘Nado’, aliyeisawazishia Azam FC kwa bao safi la kichwa.

Kiungo mashambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado, akishangilia bao lake.

Polisi Tanzania, ilirejea tena kwenye uongozi kwa bao la pili dakika ya 40, lilifungwa na Adam Adam na kufanya mpira kwenda mapumziko kwa uongozi wa mabao hayo.

Kipindi cha pili, Azam FC iliweza kutengeneza nafasi takribani mbili, lakini mashuti yaliyopigwa na Mbombo, yalipaa juu ya lango.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC, kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imejikusanyia pointi moja, iliyotokana na sare ya bao 1-1 katika mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Coastal Union.

Kiungo wa Azam FC, Paul Katema, akiwania mpira dhidi ya Tariq Seif wa Polisi Tanzania.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, leo Jumapili saa 10 Alfajiri.

Kikosi hicho kitakaporejea Dar es Salaam, mara moja kitaanza maandalizi kuelekea mchezo ujao wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) dhidi ya Pyramid ya Misri, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Oktoba 16 mwaka huu.