KIKOSI cha Klabu ya Azam FC, kimejipanga vilivyo kuondoka na ushindi wa kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2021/2022, kitakapocheza na Polisi Tanzania keshokutwa Jumamosi.

Mchezo huo wa pili wa ligi utafanyika Uwanja wa Ushirika, Moshi saa 10.00 jioni.

Azam FC ilifungua pazia la ligi ugenini kwa kuivaa Coastal Union na kutoka sare ya bao 1-1, mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi bali utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kufanya kweli na kupata matokeo bora.

Viungo washambuliaji, Idd Seleman ‘Nado’ (kushoto), akiwania mpira dhidi ya Frank Domayo ‘Chumvi’, mazoezini wakijiandaa na mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzania.

“Ukitizama jinsi ligi ilivyoanza kila timu imeanza kwenye kasi nzuri, hiyo inatupa picha sisi kuwa huko tunapoenda ni pagumu, ila sisi tunauwezo wa kupambana ili tuhakikishe tumepata matokeo mazuri tukianzia hapa Moshi,” alisema.

Azam FC tayari ipo mkoani Kilimanjaro, tayari kabisa kwa mchezo huo, kikosi kikiwa kimewasili tokea juzi Jumanne jioni, wachezaji wakionekana na ari kubwa ya kufanya vizuri katika mtanange huo.

Alisema walianza mchezo wa kwanza kwa sare ya ugenini, akidai sio matokeo mabaya kupata pointi moja ugenini.

Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina ‘Chicken’ (kushoto), akiwa na Msaidizi wake, Vivier Bahati.

“Tulikuwa na bahati mbaya tuliweza kuongoza lakini wapinzani wakasawazisha, haikuwa bahati yetu, tunaamini huko mbeleni tutakuwa na kazi nzuri,” alisema.

Ushindi wowote kwenye mchezo huo, utaifanya Azam FC kuweka kibindoni pointi nne kati ya sita za ugenini katika mechi mbili za mwanzo za ligi, takwimu ambazo ni nzuri hasa kwa mechi za ugenini.