MARA baada ya kuwasili jijini Moshi, kikosi cha Azam FC, kimeanza mazoezi rasmi leo Jumatano asubuhi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Polisi Tanzania.

Mchezo huo unatarajia kufanyika Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Ushirika jijini humo.

Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina ‘Chicken Man’, amewafanyisha mazoezi ya kuwajenga miili yao pumzi na uimara, katika mazoezi hayo ya asubuhi yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Uhifadhi Wanyapori cha Mweka.

Kikosi cha Azam FC, kikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Uhifadhi Wanyamapori Mweka.

Programu ya mazoezi itaendelea tena leo jioni, kwa wachezaji kufanyishwa mazoezi ya mpira na mbinu, tayari kabisa kujiandaa vema kuelekea mchezo huo muhimu.

Wachezajin wote wa Azam FC wako tayari kabisa kiafya kwa maandalizi ya mchezo huo, ambapo kiungo Paul Katema, aliyepata maumivu ya mguu kwenye mchezo uliopita amejiunga mazoezini na wenzake.

Azam FC ambayo huo utakuwa mchezo wake wa pili wa ligi msimu huu, ikicheza mechi zote mbili hizo ugenini, imetoka kupata sare bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, mtanange uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Vijana wa Azam FC kazini wakiipashia vilivyo Polisi Tanzania.

Matokeo hayo yameifanya kujikusanyia pointi moja katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, ambayo imeanza kwa ushindani mkubwa kwa timu zote.