KLABU ya Azam, imefungua msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani kwa pande zote mbili, ulifanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ambapo kwa matokeo hayo kila timu imejipatia pointi moja.

Azam FC iliuanza mchezo huo vema, ikifanikiwa kutengeneza nafasi takribani tano za kufunga mabao, tatu kati ya hizo akizipata mshambuliaji mpya, Idris Mbombo, ambaye alishindwa kuzitumia vema.

Kiungo Kenneth Muguna, alikuwa kwenye kiwango bora kwenye mchezo wake wa kwanza wa mashindano.

Eneo la kiungo la Azam FC, lilionekana kufanya vema, kiungo mpya wa ushambuliaji, Kenneth Muguna, akiichezesha vema timu na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao.

Muguna alionekana kushirikiana vema na viungo wenzake, Paul Katema na Sospeter Bajana, ambao nao walifanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi ya Coastal Union.

Wababe hao Chamazi, walilazimika kusubiri hadi dakika ya 49 kuweza kujipatia bao la uongozi, lililofungwa kwa kichwa na beki Daniel Amoah, akimalizia mpira uliookolewa vibaya na mabeki kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Idd Seleman ‘Nado’.

Beki Daniel Amoah, akifunga kwa kichwa bao letu la kwanza kwenye msimu mpya wa ligi.

Wenyeji Coastal Union, walisawazisha kupitia Hance Masoud, dakika ya 88.

Wakati zikiwa zimefanyika mechi tatu tu za ligi kwenye siku ya ufunguzi wa msimu, Azam FC imekaa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi moja sawa na Coastal, huku Namungo na Mbeya Kwanza walioshinda mechi zao za kwanza wakiwa nafasi ya kwanza na pili.

Kuelekea Arusha

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kuelekea mkoani Arusha kesho Jumanne saa 2.00 asubuhi, kikienda kucheza mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Polisi Tanzania, utakaofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jumamosi hii saa 10.00 jioni.