KIKOSI cha Klabu bora kabisa nchini ya Azam FC, leo Jumapili jioni kimetembelea kituo cha kulea watoto yatima, Abu-Abdul Rahman Orphanage, kilichopo jijini Tanga.

Azam FC ipo mkoani humo kwa mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Coastal Union, utakaofanyika kesho Jumatatu saa 10.00 jioni.

Msafara wa Azam FC, ukiwa kwenye picha ya pamoja na watoto na uongozi wa kituo cha Abu-Abdul Rahman Orphanage.

Msafara wote wa kikosi cha Azam FC, wakiwemo wachezaji na benchi la ufundi, wametembelea kituo hicho ikiwa ni kuwafariji na kuwasaidia watoto wanaolelewa hapo.

Katika kuwashika mkono, Azam FC imetoa msaada mdogo wa katoni za unga, sabuni, maji ya Uhai, sukari, mchele, pamoja na fedha taslimu zilizotolewa kama sadaka na walioshiriki zoezi hilo.

Mara baada ya kukabidhi kidogo hicho, uongozi wa kituo hicho pamoja na watoto walishukuru na kuiombea dua Azam FC kwenye mechi za msimu mpya wa ligi.