KIKOSI cha Klabu bora kabisa nchini ya Azam FC, kimewasili salama mkoani Tanga leo Jumamosi mchana tayari kwa mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Coastal Union.

Mchezo huo wa ufunguzi wa ligi msimu wa 2021/2022, utafanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC kiliondoka jijini Dar es Salaam alfajiri kikiwa na msafara wa wachezaji 24, benchi la ufundi na maofisa wengine wa timu.

Mshambuliaji, Idris Mbombo, akionyesha tabasamu mara baada ya kuwasili Tanga.

Wachezaji wa Azam FC wamewasili wakiwa na morali kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo, na mara kwa mara wamekuwa wakihamasishana kupambana ili kupata matokeo mazuri.

Wafanya mazoezi mepesi

Mara baada ya kuwasili mjini Tanga, kikosi hicho jioni kimefanya mazoezi mepesi ya kurudisha mwili kwenye hali yake ya kawaida (recovery).

Kikosi cha Azam FC, kikifanya mazoezi mepesi mara baada ya kuwasili mkoani Tanga.

Azam FC inatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo kesho Jumapili, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ambao utatumika kwa mtanange huo.