KIKOSI cha Azam FC kimejipanga kuanza vema msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kama kilivyomaliza msimu uliopita.

Azam FC ilimaliza vema msimu uliopita wa ligi baada ya kutopoteza mchezo wowote katika mechi 15 za mwisho, ikishinda mechi 10 na kutoka sare tano.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mchezo wa ligi, ilikuwa ni Februari 18 mwaka huu, ilipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wachezaji wa Azam FC, Daniel Amoah (kulia) na Mpianza Monzinzi, wakipambana dhidi ya wachezaji wa Coastal Union, timu hizo zilipokutana mara ya mwisho Februari 18, 2021.

Wababe hao Chamazi watafungua msimu mpya wa ligi 2021/2022 kwa kukipiga tena dhidi ya Coastal Union, mchezo ukitarajiwa kufanyika mjini Tanga Jumatatu ijayo saa 10.00 jioni.

Kuelekea mchezo huo, Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Bruce Kangwa, amesema kuwa wataanzia pale walipoishia msimu uliopita na kuongeza zaidi ili kwenda mbele.

“Unajua msimu uliopita tulianza vizuri na kumaliza kwetu tumemaliza vizuri, kwa hiyo sisi tunachukua tulipomalizia, tunaendelea tunachukua ile misimu iliyopita tunaongeza na huu msimu tuone tunafanya vipi kwenda mbele,” alisema.

Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Bruce Kangwa, akiwa mazoezini kuelekea mchezo ujao dhidi ya Coastal Union.

Alisema wameshaambiana wao kama wachezaji kuhakikisha wanapambana ili kufanya vema kwenye mchezo huo wa kwanza wa ligi.

“Sisi kama wachezaji tumejipanga vizuri wote tunajituma mazoezini, wote wanaonyesha wanataka kucheza mechi, unajua mechi ya kwanza ya ligi ndio inaonyesha mnaenda wapi,” alisema.

Kangwa aliwaomba mashabiki wa Azam FC wajitokeza kwa wingi kuwasapoti kwenye mechi zao na wao kama wachezaji watawapa matokeo wanayohitaji.

Kiungo mkabaji wa Azam FC, Sospeter Bajana, akifanya yake mazoezini kuelekea mchezo ujao dhidi ya Coastal Union.

“Mashabiki wa Azam FC tunaomba tuwe pamoja, nawaomba wote mje mjumuike pamoja na sisi mtupe sapoti mnayotupa kila siku na sisi tutawapa matokeo mnayotaka,” alimalizia.

Aidha mbali na kikosi cha Azam FC kumaliza vema ligi msimu uliopita, pia kilianza vema kwa kushinda mechi saba mfululizo huku kikiruhusu wavu wake kutikiswa mara mbili tu katika michezo hiyo, kabla ya kuwa na mwenendo mbaya na kurejea tena katika wimbi la ushindi.