KOCHA Msaidizi wa Klabu bora kabisa nchini Azam FC, Vivier Bahati, ameweka wazi kuwa watapambana kufanya vizuri ili kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC).

Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya Azam FC kuiondosha mashindanoni Horseed ya Somalia kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, ikipata ushindi katika mechi zote mbili zilizofanyika Azam Complex, ikianza kushinda 3-1 kabla ya wikiendi iliyopita kuinyuka tena 1-0.

Ushindi huo wa jumla unaifanya Azam FC kusonga mbele ya raundi ya kwanza, ambayo itakutana na matajiri wa Misri, Pyramid FC mwezi ujao.

Moja ya hekaheka langoni mwa Horseed ya Somalia, wakati Azam FC ikiichapa bao 1-0 kwenye mchezo wa marudiano.

Akizungumzia mchezo huo wa raundi ya kwanza, Bahati alisema itakuwa hatua ngumu lakini watajipanga kufanya vizuri.

“Tutajaribu kuiandaa timu vizuri ili tupate matokeo mazuri kwa uwezo wa Mungu tutapambana tufanye kazi nzuri ili tufike kwenye hatua ya makundi na ndio kitu kikubwa tunachohitaji safari hii,” alisema.

Wababe hao wa Chamazi, wataanza kuikaribisha Pyramid kwenye mchezo wa kwanza utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kati ya Oktoba 15 hadi 17, huku mchezo wa marudiano ukifanyika Misri kati ya Oktoba 22 hadi 24 mwaka huu.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akimkabili mchezaji wa Horseed ya Somalia.

Azam FC msimu huu ipo katika malengo makubwa ya kuhakikisha inaandika historia ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

Aidha kwa mara kwanza, Azam FC ilianza kushiriki michuano ya klabu barani Afrika mwaka 2013, baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2011/2012, ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.