KLABU bora kabisa nchini ya Azam, imefanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa Horseed ya Somalia bao 1-0 kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC inasonga mbele kwa raundi hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-1, kufuatia ushindi wa 3-1 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Wasomalia hao.

Wababe hao wa Chamazi, sasa watakutana na Pyramid ya Misri kwenye raundi hiyo ya kwanza, mchezo wa kwanza ukifanyika Azam Complex kati ya Oktoba 15 hadi 17 huku wa marudiano ukifanyika jijini Cairo, Misri kati ya Oktoba 22 hadi 24 mwaka huu.

Kiungo Mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Horseed.

Haikuwa kazi rahisi kwa Azam FC kusonga mbele kutokana na upinzani mkali iliouonyesha Horseed kwa dakika zote 90.

Azam FC ililazimika kusubiri hadi dakika ya ya 37 kuweza kujipatia bao hilo la ushindi lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Ismail Aziz Kader, aliyepiga shuti lilomshinda kipa wa Horseed.