KLABU bora kabisa nchini ya Azam FC, inatarajia kushuka dimbani kuivaa Horseed ya Somalia katika mchezo wa marudiano wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 10.00 jioni.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza, ambao nao ulipigwa ndani ya dimba hilo.

Licha ya kuwa nyumbani, Azam FC itakuwa ugenini kimchezo kutokana na Horseed kuchagua kutumia Uwanja wa Azam Complex katika mchezo wake wa marudiano itakaokuwa nyumbani.

Mabao ya Azam FC yaliwekwa nyavuni na Ayoub Lyanga, Idris Mbombo na beki chipukizi, Lusajo Mwaikenda, katika mchezo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa kwa pande zote mbili.

Kikosi cha Azam FC kimeshamaliza programu ya mazoezi kuelekea mchezo huo, wachezaji wakiwa na ari kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kusonga mbele kwa raundi ya kwanza.

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, akimiliki mpira mazoezini wakati wa maandalizi kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Horseed ya Somalia.

Kocha anena

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, ameweka wazi kuwa hautakuwa mchezo rahisi ila amekipanga kikosi chake kufanya vizuri uwanjani ili kuondoka na matokeo mazuri.

“Mpira uko na matokeo ya ajabu, sisi kichwani tunajua kuwa ni mechi moja ambayo itakuwa inatupa njia tunahitaji kupata matokeo mazuri, timu imeandaliwa vizuri na iko vizuri hadi kwenye mazoezi ya mwisho,” alisema.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, akiwa kwenye porogramu mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Horseed.

Bahati alithibitisha kuwa wanatarajia kuwakosa wachezaji wawili kwenye mchezo huo ambao ni majeruhi, mshambuliaji Prince Dube na kiungo mshambuliaji, Charles Zulu, anayesumbuliwa na maumivu ya enka.

Nahodha atema cheche

Naye Nahodha msaidizi wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amesema kuwa wao kama wachezaji wamejipanga vema kupata matokeo ya ushindi kwenye mchezo huo.

“Mechi ya kwanza tumepata matokeo tunamshukuru Mungu kwa hiyo mechi bado haijaisha, hii mechi ya pili tumejiandaa vizuri ili kuweza kupata matokeo,” alisema.

Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, akipenyeza pasi katikati ya wachezaji wa Horseed.

Sure Boy aliomba sapoti ya dua kwa mashabiki wa timu hiyo, akisema kuwa; “Mashabiki watusapoti kwa sababu kuja uwanjani haiwezekani, nyumbani watusapoti watuombee dua, Inshallah tutapata matokeo ya ushindi na kusonga mbele.”

Mechi hiyo itakujia mbashara kupitia kisimbuzi cha Azam TV na tutakuwa tukikupatia matokeo na kila kinachojiri uwanjani kwenye akaunti zetu za mitandao ya kijamii ya facebook na instagram.