BEKI wa kati chipukizi wa Klabu bora nchini ya Azam FC, Lusajo Mwaikenda, amesema kuwa anajifunza mengi kutoka kwa wachezaji wazoefu anaocheza nao namba moja kwenye timu hii.

Mwaikenda wikiendi iliyopita alifunga bao lake la kwanza la mashindano akiwa na kikosi hicho, wakati Azam FC ikiichapa Horseed ya Somalia mabao 3-1, kwenye mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Beki huyo kisiki, anakabiliwa na upinzani mkali kwenye namba anayocheza akipambania na wachezaji wazoefu, akiwemo Nahodha Agrey Moris, Daniel Amoah, Yvan Mballa na Abdallah Kheri Sebbo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Mwaikenda alisema amekuwa akichukua kila kilicho bora kutoka kwa wachezaji hao wakongwe ili kujijenga akiwa kama mchezaji mdogo.

“Ninajifuza mengi kwani kila mchezaji ana uzuri wake kwa hiyo ninachokifanya mimi ni kuchukua kila kilicho bora kwao ili na mimi nije kuwa bora au bora zaidi yao hapo baadaye, kwa kuwa wao wana uzoefu wa kutosha katika ligi zenye ushindani,” alisema.

Alizungumzia bao lake

Beki chipukizi, Lusajo Mwaikenda, katika moja ya hekaheka, wakati Azam FC ikiichapa Horseed ya Somalia mabao 3-1.

Beki huyo ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, chini ya Kocha Mkuu, Kim Poulsen, alizungumzia bao lake la kwanza la mashindano akiwa na uzi wa Azam FC, alilofunga dhidi ya Horeseed, akidai kuwa anajisikia furaha kuisaidia timu yake kupata ushindi.

“Kwanza najisikia vizuri kuisadia timu yangu kupata ushindi katika mchezo wa duru la kwanza pia najisikia furaha kuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga katika mchezo huo,” alisema.

Mwaikenda ni mmoja wachezaji waliolelewa kwenye kituo chetu cha kukuza vipaji cha Azam FC Academy, akipandishwa kwa mara ya kwanza timu kubwa miaka mitatu iliyopita, kabla ya kutolewa kwa mkopo KMC na kurejea msimu huu.

Beki huyo anayesifika kwa matumizi mengi ya akili na kucheza kwa ustadi mkubwa mipira ya juu na chini, alikuwa ni mchezaji wa kutumainiwa kwenye eneo la ulinzi akiwa KMC, ambako alifanikiwa kufunga jumla ya mabao matatu katika ligi.