VIUNGO washambuliaji wa Klabu bora nchini ya Azam FC, Ayoub Lyanga na Idd Seleman ‘Nado’, wameandika rekodi muhimu katika mechi ya kwanza kwenye msimu mpya wa mashindano 2021/2022 dhidi ya Horseed ya Somalia.

Wachezaji hao wameandika rekodi ya klabu msimu huu, wakati Azam FC ikiichapa Horseed ya Somalia mabao 3-1 katika mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, uliofanyika Uwanja wa Azam Complex wikiendi iliyopita.

Nado na Lyanga, wakipongezana na wachezaji wenzao baada ya Azam FC kufunga bao la kwanza dhidi ya Horseed ya Somalia.

Lyanga anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao letu la kwanza la msimu kwenye msimu mpya wa mashindano 2021/2022, huku Nado aliyemmegea pande akiwa mchezaji wa kwanza kutoa pasi ya kwanza iliyozaa bao (assisti), aliyoitoa kwa mpira wa adhabu ndogo alioupiga dakika ya 32 na Lyanga kuujaza wavuni kwa kichwa safi.

Mabao yetu mengine katika mchezo huo, yalifungwa na mshambuliaji mpya Idris Mbombo na beki chipukizi, Lusajo Mwaikenda, ambao wote walikuwa wakifunga mabao yao ya kwanza wakiwa na uzi wa Azam FC.

Msimu uliopita ilikuaje?

Msimu uliopita 2020/2021, mechi ya kwanza ya msimu ya Azam FC ilikuwa ni ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, Septemba 7, 2020, ikishinda bao 1-0 huku mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Obrey Chirwa, akiandika rekodi ya kufunga bao la kwanza la msimu kwa matajiri hao.

Chirwa alitupia bao hilo dakika ya 44 kwa kichwa kama alivyofunga Lyanga msimu huu, akiunganisha krosi safi iliyopigwa na mshambuliaji hatari, Prince Dube, ambaye naye alitoa pasi ya kwanza iliyozaa bao kwenye msimu huo mpya.

Lyanga, Nado wafunguka

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Lyanga alisema kuwa anajisikia furaha kufunga bao la kwanza la Azam FC msimu huu huku akidai furaha yake imeongeza zaidi kutokana na umuhimu wa bao hilo.

“Najisikia furaha zaidi kufunga kuweza kufunga bao ambalo limeturudisha katika ari ya ushindi naamini itakuwa hivyo katika mashindano yote tutakayokuwa tunacheza itakuwa ni mwendelezo wa ushindi katika timu yangu,” alisema.

Lyanga amesema bao hilo limempa mwanzo mzuri wa msimu, akiongeza kuwa; “Nimejipanga vizuri kuipigania timu yangu Azam FC kuelekea msimu wa Ligi Kuu na mashindani mengine, katika kufunga na kutoa mchango kwa timu yangu ili kuweza kufikia malengo ya timu yangu kwa ujumla.”

Kiungo mshambuliaji huyo aliyetua Azam FC msimu uliopita, alikuwa na msimu mzuri uliopita baada kufunga jumla ya mabao nane na pasi tatu zilizozaa mabao kwenye ligi.

Nado akifanya yake wakati Azam FC ikifungua mechi ya kwanza ya mashindano msimu 2021/22 dhidi ya Horseed ya Somalia.

Naye Nado alisema kuwa atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anaipigania Azam FC akizidisha kile alichokifanya kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Horseed.

“Namshukuru mwenyezi Mungu nimeanza vizuri na nitajitahidi zaidi na zaidi kadiri ya uwezo wangu kuelekea mechi zinazokuja katika kuisaidia timu yangu,” alisema.

Msimu uliopita, Nado aliandika rekodi ya kipekee, akiwazidi wachezaji wote wazawa nchini, baada ya kuhusika katika jumla ya mabao 19 ndani ya ligi, akifunga 10 na kutoa pasi za mwisho tisa.