KIKOSI cha klabu ya Azam FC, kinatarajia kuingia kambini leo Jumatatu jioni kwa ajili ya kujiwinda na mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed ya Somalia.

Azam FC inaingia kambini baada ya mapumziko ya siku moja jana Jumapili, kufuatia ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Wasomalia hao, uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Kiungo mshambuliaji, Idd Seleman ‘Nado’, akijaribu kumtoka beki wa Horseed katika mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo wa marudiano wa raundi ya awali ya michuano hiyo unatarajia kupigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 10.00 jioni, baada ya Horseed kuchagua kuchezea Tanzania mechi yake hiyo ya nyumbani.

Wachezaji wote wanatarajia kuingia kambini, isipokuwa mshambuliaji Prince Dube, ambaye ametoka kwenye matibabu jijini Cape Town, Afrika Kusini, alikofanyiwa upasuaji mdogo katika Hospitali ya Vincent Palloti.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, aliyekuwa nje ya dimba kwa muda wa wiki mbili, naye ameshapona majeraha ya mguu yaliyokuwa yakimkabili baada ya kujiunga mazoezini na wenzake Alhamisi iliyopita, tayari kujiandaa na mechi za ushindani.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, tayari amerejea mazoezini baada ya kupona majeraha ya mguu.

Naye kiungo mshambuliaji, Ayoub Lyanga, aliyeumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Horseed, anatarajia kufanyia uchunguzi zaidi wa jeraha lake leo ili kujua undani wa tatizo lake.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, ameshaweka wazi kuwa watacheza kwa tahadhari kubwa kwenye mchezo huo wa marudiano, licha ya Horseed kuchezea mechi hiyo Tanzania.