KOCHA Msaidizi wa Klabu ya Azam FC, Vivier Bahati, amesisitiza kuwa mpira wa kisasa hauna cha kuchezea nyumbani ili kupata matokeo, hivyo kikosi chake kitaingia kwa tahadhari kubwa kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Horseed ya Somalia.

Mchezo huo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, nao utafanyika nchini kwenye Uwanja wa Uhuru Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni, baada ya Horseed kuchagua kutumia uwanja huo katika mechi yake ya nyumbani.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na akiba ya ushindi wa mabao 3-1 iliupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jana Jumamosi usiku.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akichanja mbuga kuelekea langoni mwa Horseed.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, Bahati alisema kikosi chake kucheza nyumbani hakuwapi nafasi ya kusonga mbele bali kitu pekee wanachofaidika nacho ni kutosafiri kuwafuata wapinzani hao kwao.

“Suala la uwanjani mpira ni dakika 90 chochote kinaweza kutokea ila ni sisi kujiandaa kwenye mechi ya pili ili kufanya vizuri,” alisema Bahati.

Mabao ya Azam FC kwenye mchezo wa kwanza yaliwekwa kimiani na kiungo mshambuliaji Ayoub Lyanga, mshambuliaji mpya Idris Mbombo na beki wa kati chipukizi, Lusajo Mwaikenda.

Akizungumzia mchezo, alisema kikosi chake kimejitahidi kucheza na kupata mabao licha ya kumaliza maandalizi ya msimu ‘Pre season’ hivi karibuni.

“Sisi tulikuwa na hali ya utulivu ya kutafuta matokeo bahati mbaya tukaruhusu bao la mapema kwenye mpira wa kutengwa, kipindi cha kwanza tulipata sehemu nzuri za kumalizia lakini hatukuwa watulivu ndani ya boksi kama tungekuwa watulivu tungepata mabao mapema.

“Tumevumilia hadi mwisho ile hali ya kushambulia pembeni ndio tulikuwa tumeandaa basi na ikatupatia matokeo mazuri,” alisema.

Aidha aliongeza kuwa kwa sasa kikosi chake kinahitaji muda ili wachezaji wapya waliosajiliwa kuweza kuelewana kiuchezaji na wachezaji wa zamani.

“Inabidi tuwape muda ukitizama Nado na Mbombo sio muda mrefu wako pamoja, ila Nado na Dube (Prince) walikuwa muda mrefu na wamezoeana, naamini Nado na Mbombo nao tukiwapa muda nao watazoeana na zile nafasi atakazotengeneza Mbombo atzitumia na kufanya vizuri,” alimalizia.