KIKOSI cha Azam FC kimeanza vema michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuichapa Horseed ya Somalia mabao 3-1 kwenye mchezo wa raundi ya awali uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumamosi usiku.

Huo ni mchezo wa kwanza wa mashindano kwa Azam FC msimu huu, ikiwa imeanza na ushindi mnono.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akimtoka beki wa Horseed ya Somalia.

Mpira ulianza kwa kasi, Azam FC ikifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Horseed kupitia pembeni kwa viungo washambuliaji, Ayoub Lyanga na Idd Seleman ‘Nado’, lakini jitihada zao ziliishia kwenye safu ya ulinzi ya Wasomalia hao.

Horseed ilicharuka na kupata bao la uongozi dakika ya 23, likifungwa na Ibrahim Nor, kwa mpira wa adhabu ndogo uliogonga ukuta na kumpoteza kipa, Mathias Kigonya.

Azam FC iliamka na kujibu mashambulizi, hatimaye ilifanikiwa kusawazishia bao hilo dakika ya 32 likifungwa kwa kichwa na Lyanga, akimalizia mpira wa adhabu ndogo pembeni uliochongwa na Nado.

Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ametoa pasi ya mwisho kwenye mechi ya kwanza ya mashindano msimu huu.

Mabadiliko ya dakika ya 70 ya kuingia kiungo Paul Katema na kutoka Mudathir Yahya, yaliongeza uhai kwenye eneo la kiungo la Azam FC na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyohitimisha ushindi huo mnono.

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Idris Mbombo, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya mashindano, dakika ya 73 aliifungia timu hiyo bao la pili kwenye mchezo akimchambua kipa wa Horseed na kujaza mpira kimiani, akitumia vema pasi ya juu ya kiungo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.  

Hilo linakuwa bao la kwanza la Mbombo akiwa na uzi wa Azam FC, tokea asajiliwe msimu huu.

Mshambuliaji wa Azam FC, Idris Mbombo, amefunga bao lake la kwanza akiwa na uzi wa Azam FC.

Mpira wa kona uliochongwa na Nado dakika 78, ulizua kizaazaa langoni mwa Horseed, baada ya mpira kumkuta Lyanga, aliyepiga shuti kali lililogonga mwamba wa pembeni kabla mpira kudondokea kwa beki Lusajo Mwaikenda, aliyeujaza wavuni na kuiandikia Azam FC bao la tatu.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kutanguliza mguu mmoja kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, kwani itahitaji kulinda ushindi wake huo katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Septemba 18, mwaka huu saa 10.00 jioni.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitapumzika kesho Jumapili kabla kuanza rasmi maandalizi ya mtanange wa marudiano keshokutwa Jumatatu saa 10.00 jioni.

Mshindi wa jumla wa mechi zote mbili, atakutana na matajiri wa Misri, Pyramid, kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, mechi zitakazofanyika Oktoba mwaka huu.