KLABU bora kabisa nchini, Azam FC, itafungua msimu wake wa mashindano wikiendi hii kwa kucheza dhidi ya Horseed ya Somalia.

Mchezo huo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika utafanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumamosi saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo kikiwa chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina ‘Chicken’ na Msaidizi wake, Vivier Bahati.

Kiungo wa Azam FC, Never Tigere, akimtoka Tepsie Evance, wakati wa maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Horseed kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mara baada ya mchezo huo, Horseed imechagua kurudiana na Azam FC hapa chini katika mchezo wake wa nyumbani ikitumia Uwanja wa Uhuru, mchezo utakaofanyika kati ya Septemba 17 hadi 19.

Kuelekea mchezo huo wa kwanza, Azam FC tunakuletea takwimu za jumla za timu yako pendwa kihistoria kwenye michuano hiyo.

Safari ya Azam FC Kombe la Shirikisho Afrika

Kihistoria Azam FC ilianza kushiriki michuano ya kimataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 2013, baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2011/2012.

Februari 16, 2013, Azam FC ikaanza kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ikikipiga dhidi ya Al Nasir ya Juba, Sudan Kusini, kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika nyumbani, Azam FC ilishinda mabao 3-1.

Mabao ya wenyeji yakiwekwa kimiani na Kipre Tcheche, aliyefunga mawili (80’, 90’) huku kiungo Abdi Kassim ‘Babbi’ akitupia jingine (15’).

Mchezo wa marudiano uliopigwa Juba, Machi 3, 2013, Azam FC iliandikisha ushindi mwingine mnono ikiichakaza Al Nasir 5-0, huku Khamis Mcha ‘Vialli’ akiibuka kidedea baada ya kutupia hat-trick (25’, 31’, 70’), Tchetche (60’) na John Bocco (49’) wakifunga mengine. Azam FC ikisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 8-1.

Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche, akimtoka mlinzi wa Al Nasir ya Juba kwenye Uwanja wa Mkapa.

Raundi ya kwanza: Azam FC ikapangwa kucheza na Barrack Young Controllers II ya Liberia kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, ikianzia ugenini Monrovia, Machi 17, 2013 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, yaliyofungwa na Humphrey Mieno (55’) na Seif Abdallah ‘Karihe’ (89’).

Kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Mkapa (zamani Taifa), jijini Dar es Salaam, Azam FC ililazimishwa suluhu na hivyo kusonga mbele kwa raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 ilioupata ugenini.

Raundi ya pili: Azam FC ilipangwa kukipiga dhidi ya FAR Rabat ya Morocco kwenye raundi ya pili ya michuano hiyo, ikianzia nyumbani Uwanja wa Mkapa, Aprili 20, 2013 na kutoka suluhu.

Azam FC ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo, Mei 04, 2013, iliweza kujitutumua ugenini jijini Rabat kwa kufungwa mabao 2-1, huku mshambuliaji Bocco akikosa penalti muhimu dakika za mwisho ambayo kama angeipata ingeivusha Azam FC kwenda raundi ya mwisho ya mtoano (play off round).

Wababe hao wa Chamazi, ambao walicheza pungufu ya watu wawili uwanjani baada ya David Mwantika na Wazir Salum kuonyeshwa kadi nyekundu, kama Bocco angepata penalti hiyo basi Azam FC ingetoka sare ya mabao 2-2, na ingesonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.

Mwaka 2014: Huku ikishiriki michuano ya Afrika kwa mara ya pili kihistoria, huu mwaka Azam FC ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi msimu wa 2012/2013.

Ndio ulikuwa mwaka wa kwanza, Azam FC kutumia uwanja wake wa Azam Complex, kama uwanja wa nyumbani kwenye michuano hiyo ya Afrika baada ya kukidhi viwango vya kimataifa.

Ilikuwa bahati mbaya kwa Azam FC, kwani iliweza kutolewa raundi ya awali na Ferroviário da Beira ya Msumbiji, kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

Wachezaji wa Azam FC wakiwa kwenye moja ya harakati langoni mwa Ferroviário da Beira kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mechi ya kwanza iliofanyika Azam Complex, Februari 9, 2014, Azam FC ilishinda bao 1-0, lililofungwa na Tchetche dakika ya 41, huku mchezo wa marudiano uliopigwa mjini Beira Februari 16, Ferroviário ilishinda 2-0.

Mwaka 2015: Huu ndio mwaka pekee ambao Azam FC ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa taji la ligi msimu wa 2013/2014 bila kupoteza mchezo wowote kihistoria.

Azam FC ikaishia raundi ya awali kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa na El Merreikh ya Sudan kwa ushindi wa jumla wa 3-2, mechi ya kwanza iliyofanyika Azam Complex Februari 15, 2015, Azam FC ilishinda 2-0, mabao yakifungwa na Didier Kavumbagu (9’) na John Bocco (71’). Mchezo wa marudiano uliofanyika jijini Khartoum Februari 28, Merreikh ilishinda 3-0.

Mwaka 2016: Azam FC ilirejea tena kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi msimu wa 2014/2015, mwaka ambao Azam FC ilijaribu kufanya makubwa tena kwenye michuano hiyo ya Afrika baada ya kuishia raundi ya pili.

Raundi ya Kwanza: Tofauti na miaka mingine, safari hii Azam FC haikucheza raundi ya awali, ilipangwa kuanzia raundi ya kwanza, ambapo ilikutana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kuitoa kwa ushindi wa jumla wa 7-3.

Mshambuliaji Kipre Tchetche, akimtungua kipa wa Bidvest Wits kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC ilianzia ugenini Machi 12, 2016 jijini Johanesburg dhidi ya Bidvest, na kupata ushindi wa mabao 3-0, yaliyofungwa na Bocco (61’), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (51’) na Shomari Kapombe (56’).

Mechi ya marudiano iliyopigwa Azam Complex Machi 20, 2016, Azam FC ilipata ushindi mwingine wa 4-3, Tchetche akiibuka kidedea kufunga hat-trick (23’, 55’, 88’), huku Bocco akitupia jingine (41’).

Raundi ya pili: Azam FC baada ya kuwatoa Wasauzi hao, ikapangwa kukipiga dhidi ya Esperance ya Tunisia kwenye raundi ya pili ya michuano hiyo, na kutolewa kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2.

Winga wa Azam FC, Farid Mussa, akijaribu kuwatoka wachezaji wa Esperance ya Tunisia kwenye Uwanja wa Azam Complex

Azam FC ilianza kwa ushindi wa 2-1 nyumbani Azam Complex Aprili 10, 2016, mabao yakiwekwa kambani na Farid Mussa (69’) na Ramadhan Singano ‘Messi’ (70’), lakini ikapoteza ugenini kwa ushindi wa 3-0 wa Esperance Aprili 19, 2016.

Mwaka 2017: Azam FC ikashiriki tena Kombe la Shirikisho Afrika baada ya msimu wa 2015/2016 kumaliza kama washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), ikifungwa kwenye fainali na Yanga mabao 3-1

Raundi ya kwanza: Azam FC haikupangwa tena kuanza raundi ya awali kwenye michuano hiyo, ikaanzia raundi ya kwanza kwa kupangiwa Mbabane Swallows ya Eswatini, ambayo ilisonga mbele kwa raundi ya mwisho ya mtoano (play offs) kwa ushindi wa jumla wa 3-1.

Azam FC ilianzia nyumbani Azam Complex Machi 12, 2017 na kushinda 1-0, bao lililofungwa dakika ya 85 na Ramadhan Singano ‘Messi’, huku ikipoteza ugenini Machi 19, 2017 kwa kufungwa 3-0.

Mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Chilunda, akimiliki mpira mbele ya Papy Tshitshimbi wa Mbabane Swallows.

Ikapotea misimu miwili CAF

Azam FC ikapotea kwenye michuano ya Afrika kwa misimu miwili, hadi iliporejea tena mwaka 2019 baada ya msimu wa 2018/2019 kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu 2019/2020: Wakati ikirejea kwa mara nyingine kwenye michuano ya Afrika, Azam FC ikapangwa kucheza na Fasil Kenema ya Ethiopia kwenye raundi ya awali na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-2.

Mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa, akimtoka nahodha wa Fasil Kenema ya Ethiopia, kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC ilianza kwa kupoteza bao 1-0 ugenini Agosti 11, 2019 kabla ya kutakata nyumbani Azam Complex Agosti 24, 2019 kwa ushindi wa 3-1, mawili yakifungwa na Richard Djodi (23’, 32’) na jingine likifungwa na Obrey Chirwa (59’).

Raundi ya kwanza: Baada ya kuitoa Kenema, Azam FC ikapangiwa Triangle ya Zimbabwe kwenye raundi ya kwanza, lakini haikuwa bahati nzuri kwa Wababe hao wa Chamazi baada ya kupoteza mechi zote mbili, kwa bao 1-0 nyumbani na ugenini, na Triangle ikasonga mbele kwa mabao 2-0.

Azam FC imerejea tena kimataifa:

Baada ya kupotea kwa msimu mmoja kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika, msimu huu Azam FC imerejea tena kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na malengo ya kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Katika kujiandaa vema na michuano hiyo na msimu mpya, kikosi cha Azam FC kiliweka kambi ya wiki mbili jijini Ndola, Zambia na kucheza mechi tatu za kimataifa za kirafiki na timu za huko.

Mchezo wa kwanza ilianza kupoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya Red Arrows kabla ya mechi iliyofuata kuichapa Kabwe Warriors bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube huku mtanange wa mwisho ikiwachapa mabingwa wa Zambia, Zesco United bao 1-0, lililowekwa nyavuni na mshambuliaji mpya Roger Kola.

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Roger Kola, akifanya yake dhidi ya Zesco United kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Ikiwa imejipanga vilivyo na kufanya usajili mzuri, Azam FC itaanza kucheza na Horseed na mshindi wa jumla atakutana na Pyramid ya Misri kwenye raundi ya kwanza mwezi ujao.