KIKOSI cha Azam FC kimekamilisha kambi ya siku 14 jijini Ndola, Zambia kwa kuwachapa mabingwa wa nchi hiyo, Zesco United bao 1-0 kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, Azam FC ikionekanba kuimarika vilivyo tofauti na mechi mbili zilizopita, wachezaji wakionyesha ari kubwa ya ustahimilivu wa kupambana.

Bao pekee la Azam FC limewekwa kimiani dakika ya 54 na mshambuliaji mpya Roger Kola, dakika ya 54 akiunganisha kwa mguu shuti kali lililopigwa na kiungo Paul Katema, ndani ya eneo la 18.

Kola aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Frank Domayo, alionekana kuisumbua mno safu ya ulinzi ya Zesco United, akionesha uwezo mzuri wa kukaa na mipira na kucheza mipira ya juu, akishirikiana vema na mshambuliaji mwingine, Idris Mbombo.

Mbinu za Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina, za kuchezesha washambuliaji wawili kipindi cha pili zilionekana kumlipa, hasa baada ya kuimarika kwa eneo la kushambulia kutokana na mashambulizi mengi kuleta hatari kwenye lango la Zesco United.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Ismail Aziz, akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Zesco United.

Safu ya ulinzi iliyokuwa imeundwa na mabeki wa kati Daniel Amoah na beki mpya wa kati, Yvan Mballa, ilionekana kucheza vema wakisaidiwa na mabeki wa pembeni nahodha Bruce Kangwa na Abdul Omary (Nickolas Wadada kipindi cha pili), ambao nao walifanya kazi kubwa kupunguza makali ya Zesco United pembeni ya uwanja.

Kipa Mathias Kigonya, alifanya kazi kubwa sana kuokoa michomo mingi na krosi za wachezaji wa Zesco United, waliokuwa wakiongozwa na mshambuliaji wao kinara Jesse Were, ambaye alipumzishwa kipindi cha pili.

Sehemu ya kiungo ya Azam FC, ambayo kipindi cha kwanza ilianza na Domayo, Sospeter Bajana na Katema, nayo ilionekana kuimarika tofauti na mechi zilizopita, hata alipoingia Never Tigere, kipindi cha naye alionekana kusaidia eneo la kushambulia, ambapo dakika ya 50 aliweza kupiga mpira wa adhabu ndogo uliogonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki.

Hiyo ni mechi ya pili ya kimataifa ya kirafiki kwa Azam FC kushinda, baada ya awali kuwachapa washindi wa nne wa Ligi Kuu ya Zambia, Kabwe Warriors bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji Prince Dube, kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Domayo

Ushindi wa mechi hizo mbili, ulitanguliwa na kupoteza mchezo wa kwanza wa kirafiki, ikifungwa mabao 4-0 ilpocheza na washindi wa tatu wa ligi hiyo, Red Arrows.

Kocha Lwandamina maarufu kama Chicken Man au Professor, ameweka wazi kuwa kwa sasa anachoangalia kwenye kikosi chake hivi sasa ni kuwaweka fiti na kutengeneza ustahimilivu na spidi kwa wachezaji wake kabla ya kuhamia katika hatua ya mwisho ya mbinu.

Kurejea Tanzania

Mara baada ya mchezo huo wa mwisho dhidi ya Zesco United, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar Es Salaam, Tanzania keshokutwa Jumapili asubuhi na kikitarajia kufika Jumatatu usiku, tayari kuendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Horseed ya Somalia katika mchezo wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC itacheza mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, Septemba 11 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, huku mchezo wa marudiano ukipigwa Uwanja wa Uhuru kati ya Septemba 17 hadi 19 mwaka huu.