KIKOSI cha Azam FC kinatarajia kuhitimisha kambi ya siku 14 jijini Ndola, Zambia kwa kucheza mchezo wa mwisho wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa Zambia, Zesco United.

Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa kesho Alhamisi saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, ukiwa ni wa tatu kwa kikosi hicho kikiwa kambini nchini humo.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina, mara baada ya kumalizika kwa mchezo uliopita dhidi ya Kabwe Warriors na kushinda bao 1-0, limeelezea kuimarika kwa kikosi hicho ukilinganisha na mechi ya kwanza waliyopoteza walipocheza na Red Arrows.

Beki wa Azam FC, Daniel Amoah, akimiliki mpira mbele ya beki mwenzake, Abdallah Kheri, mazoezini leo Alhamisi asubuhi.

Wachezaji wa Azam FC wakiwa kambini jijini Ndola, wamekuwa wakifanyishwa programu ya mazoezi ya utimamu wa mwili, spidi na kuchezea mpira kidogo, ikiwa ni sehemu ya kuwekwa fiti ili kuwa na ustahimilivu wa kupambana wakiwa uwanjani kwenye mechi za mashindano zinazoanza mwezi huu.

Kocha Lwandamina ‘Chicken Man’, atakiongoza kikosi chake kucheza mchezo huo dhidi ya timu yake ya zamani, aliyoifundisha na kupata nayo mafanikio kwa nyakati tofauti kabla ya kutua Azam FC Novemba mwaka jana.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, Tanzania, Jumapili hii mchana, tayari kuendelea na programu mwisho mwisho kabla ya kucheza mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed ya Somalia kwenye Uwanja wa Azam Complex, Septemba 11, mwaka huu.