KLABU ya Azam imekamilisha taratibu za kumsajili beki wa kati raia wa Cameroon, Yvan Lionnel Mballa, kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Forest Rangers ya Zambia.

Mballa, 27, aliyesaini mkataba mbele ya Meneja wa timu, Luckson Kakolaki, anakuja kuongeza nguvu kwenye eneo la ulinzi la Azam FC kuelekea msimu mpya unaotarajia kuanza kutimua vumbi wiki chache zijazo.

Beki wa kati, Yvan Lionnel Mballa, akisaini mkataba wa kujiunga Azam FC mbele ya Meneja wa timu, Luckson Kakolaki.

Beki huyo anayetumia kwa ufasaha mguu wa kushoto, ameshajiunga na wachezaji wenzake kambini jijini Ndola, Zambia tayari kwa maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kikosi hicho hakijarejea jijini Dar es Salaam, Tanzania Jumatatu ijayo.

Huo unakuwa ni usajili wetu wa nane kwa wachezaji wapya kwenye dirisha hili la usajili na tunahitimisha rasmi zoezi hilo katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo.

Wachezaji wengine tuliowasajili ni kipa Ahmed Salula, beki wa kushoto Edward Manyama, kiungo mkabaji Paul Katema, viungo washambuliaji Kenneth Muguna, Charles Zulu na washambuliaji, Rodger Kola na Idris Mbombo.