MSHAMBULIAJI Prince Dube, ameiongoza Azam FC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kabwe Warriors.

Mchezo huo wa maandalizi ya msimu mpya unaotarajiwa kuanza Septemba mwaka huu, ulifanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola, Zambia.

Dube aliyeingia dakika ya 55 kuchukua nafasi ya Rodgers Kola, alitumia dakika mbili tu kuweza kuandika bao hilo pekee la Azam FC kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’.

Bao hilo linamfanya mshambuliaji huyo kinara kurejea na moto wake wa kufumania nyavu aliokuwa nao msimu uliopita, akifanikiwa kuwa mfungaji bora wa Azam FC baada ya kuzifumania nyavu za wapinzani mara 17 katika mashindano yote.  

 Tofauti na mchezo uliopita dhidi ya Red Arrows, kikosi cha Azam FC kimeonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, miili ya wachezaji ikionekana kuanza kufunguka taratibu baada ya programu ya mazoezi ya spidi na utimamu wa mwili kuanza kuwaingia vizuri.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Ismail Aziz, akimiliki mpira mbele ya beki wa Kabwe Warriors.

Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina, ameshaweka wazi kubwa bado anaendelea na programu ya mazoezi makali kwa wachezaji yake, ili kuwaandaa vema kiufiti na spidi, kuelekea msimu mpya.

Mara baada ya mchezo huo wa pili wa kimataifa wa kirafiki, kikosi cha Azam FC kitashuka tena dimbani Septemba 03 mwaka huu kucheza na mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia na Kombe la Shirikisho (FA Cup), Zesco United.

Mchezo huo unatarajia kuhitimisha kambi ya maandalizi ya Azam FC nchini Zambia.