WAKATI kikosi cha Azam FC kikiendelea na kambi jijini Ndola, Zambia, kesho Jumapili kitashuka tena dimbani kujipima dhidi ya Kabwe Warriors kwenye mchezo wa pili wa kimataifa wa kirafiki.

Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa, saa 9.00 Alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, Kocha Mkuu, George Lwandamina, akiutumia kama sehemu ya kuwaangalia wachezaji namna wanavypokea programu ya mazoezi anayowapa.

Kikosi hicho kipo nchini humo kwa kambi ya maandalizi kuelekea msimu huu unaotarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia mwezi ujao, Azam FC pia ikiwa na kalenda ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mshambuliaji Prince Dube (kushoto), ni mmoja wachezaji waliofanya mazoezi ya mwisho leo Jumamosi kabla ya kuivaa Kabwe Warriors.

Lwandamina ameweka wazi kuwa kwenye maandalizi hayo kwa sasa haangalii matokeo ya uwanjani, bali anaangalia utimamu wa mwili kwa wachezaji wake na spidi, kwani ndio program anayoifanyia kazi kwa sasa kabla ya kuhamishia nguvu katika mazoezi ya mpira (ufundi zaidi).

Katika mchezo wa kwanza wa kirafiki kikosi hicho kikiwa kambini hapa, Azam FC ilipoteza kwa mabao 4-0 dhidi ya Red Arrows, ambayo imeanza kwa muda mrefu maandalizi yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu Zambia.

Azam FC ikiwa jijini Ndola, inawakosa wachezaji wake nane, saba wakiwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kipa Wilbol Maseke, mabeki Lusajo Mwaikenda, Edward Manyama, viungo washambuliaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Idd Seleman ‘Nado’ na Ayoub Lyanga, huku Agrey Moris, akiwa majeruhi.

Kiungo Kenneth Muguna, atajiunga na timu yake ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, mara baada ya kucheza na Kabwe Warriors.

Mchezaji mwingine ambaye yuko jijini Ndola, ambaye anatarajia kujiunga timu ya Taifa, ni kiungo mshambuliaji Kenneth Muguna, akitarajiwa kujumuika kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ mapema wiki ijayo.